Maofisa wa Korea zote mbili kukutana juu ya kuzungumzia maswala muhimu ya Ushirikiano

So Se Pyong Balozi wa Korea Kaskazini kwenye Umoja wa Mataifa
So Se Pyong Balozi wa Korea Kaskazini kwenye Umoja wa Mataifa

Maofisa wa Korea Kaskazini na Korea Kusini leo jumatano wanafanya mkutano mkubwa wa kwanza kuzikutanisha pande hizo mbili, unaoangazia maswala muhimu ya ushirikiano kabla ya kufanyika kwa shughuli muhimu ya kuwakutanisha watu wa familia zilizotenganishwa na vita vya Korea miaka sitini iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano wa hii leo unafanyika kwenye eneo la mpaka katika kijiji cha Panmunjom huku jambo linalotarajiwa kupewa kipaumbele zaidi ni tukio la kuzikutanisha familia hizo lililopangwa kufanyika kati ya tarehe 20 hadi 25 mwezi huu.

Huenda Pyongyang ikatumia nafasi hiyo kushishinikiza majirani zao kuahirisha mazoezi ya kijeshi baina yao na Marekani yanayotarajiwa kuanza tarehe 24 mwezi huu.

Kumekuwa na hofu huenda Korea Kaskazini ikaahirisha kushiriki tukio la kuziunganisha familia ikiwa Korea Kusini na Marekani wataendelea na mpango wa kushiriki mazoezi ya kijeshi baadaye mwezi huu.

Vita baina ya Korea Kaskazini na Kusini miaka sitini iliyopita ilimalizika kwa kusitishwa mapigano na sio makubaliano ya amani, hatua ambayo haikumaliza uadui baina ya Mataifa hayo jirani.