SYRIA

Machafuko zaidi yaripotiwa katika miji ya Homs na Hama nchini Syria

Waandamanaji nchini Syria wakiandamana baada ya sala ya Ijumaa
Waandamanaji nchini Syria wakiandamana baada ya sala ya Ijumaa Reuters/Handout

Watu zaidi ya watu 44 wameripotiwa kuuawa na Polisi nchini Syria katika miji ya Homs, Hama na Deraa ambako kulifanyika maandamano makubwa siku ya ijumaa kushinikiza kujiuzulu kwa rais Bashar al-Asad.

Matangazo ya kibiashara

Waandaaji wa maandamano ya Ijumaa waliyaita maandamano hayo endelevu mpaka pale utawala wa rais Asad utakapotangaza kuondoka madarakani na kupisha utawala wa demokrasia nchini humo.

Siku ya Alhamisi wanaharakati na wanasiasa wa vyama vya Upinzani nchini Syria walikutana nchini Uturuki na kuunda baraza maalumu ambalo litasimamia maandamano hayo kwa kuomba msaada toka jumuiya ya kimataifa.

Rais Bashar al-Asad ameendelea kusisitiza serikali yake kusalia madarakani na kwamba ni kwa njia ya mazungumzo pekee ndio itakayoweza kumaliza mzozo wa kisiasa uliko nchini humo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akiongea na waandishi wa habari siku ya Ijumaa amesema kuwa anasikitishwa na hali inavyoendelea nchini Syria na kwamba anashangazwa na rais Asad kwa kutotimiza ahadi yake aliyomwambia ya kusitisha machafuko nchini mwake.