Syria

Marekani yachachamaa kwa balozi wake nchini Syria kushambuliwa kwa mayai

RFI

Serikali ya Marekani imelaani vikali hatua ya Balozi wake nchini Syria Robert Ford kushambuliwa kwa mayai na wafuasi wa Rais Bashar Al Assad ambao wamekwera na hatua yake ya kukutana na Vyama vya Upinzani huko Damascus.

Matangazo ya kibiashara

Wafuasi wa Rais Assad wanaokadiriwa kufikia mia moja wakiwa na hasira waliamua kumshambulia Balozi Ford akiwa kwenye harakati zake za kukutana na upinzani wakidai Marekani inachochea machafuko.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema shambulizi hilo halistahili kufanywa kwa Balozi Ford kwani alikuwa anafanya shughuli zake zinazotambulika kimataifa.

Marekani imesema kuwa shambulizi hilo kwa balozi wake ni mwendelezo wa jitihada za wafuasi wa Rais Assad kuendelea kuwatisha na kuwanyanyasa wanadiplomasia walioko nchini Syria ili wasiendelee na jitihada za kuleta amani.

Marekani imetoa wito kwa Serikali ya Syria kuhakikisha inawalinda wanadiplomasia waliomo nchini humo kwa kufuata sheria za kimataifa.

Waziri Clinton amesema kuwa kutokana na shambulizi hilo, Marekani haitamrudisha nyumbani balozi Ford na amelitaka baraza la seneti kumuidhinisha tena balozi huyo ili aendelee na kazi zake nchini Syria.