Wanaharakati zaidi ya kumi wauwawa Syria.
Wanaharakati zaidi ya kumi wanaompinga rais wa Syria wameuawa katika purukushani za Ijumaa hii nchini Syria katika harakati za kuwaunga mkono wanajeshi wa Syria waliojiunga na makundi ya watu wanaomtaka rais Bashar Al Assad kuachia ngazi.
Imechapishwa:
Mashirika yanayo tetea haki za binadamu yamethibitisha kuwa idadi kubwa ya wanajeshi wamejiunga na wanaharakati katika madai hayo dhidi ya mtawala wao.
Wanaharakati hao walitoa ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook ukiwataka wafuasi wake kuandamana juu ya kile walichokiita mwanajeshi aliehuru. Hii ni baada ya kutokea mauaji ya watu 36, 26 kati yao wakiwa ni wanajeshi katika mashambulizi ya huku na kule nchini humo.
Kamishna mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Nevy Pillay amesema katika taarifa yake kwamba idadi ya waliouawa imezidi watu elfu tatu, mia moja na thamanini na saba kati ya hao, ni watoto, tangu pale yalipoanza mapambano ya wanaharakati na vikosi vya usalama.
Watu zaidi ya mia moja wameuawa katika siku kumi za nyuma, huku wengine wakikamatwa na kuendesha vitendo vya kikatili.