Mapigano makali yaripotiwa mpakani mwa Uturuki na Iraq
Mapigano makali yameripotiwa katika mpaka wa nchi ya Uturuki na Iraq baada ya majeshi ya Uturuki kuingia nchini Iraq kuwasaka wanamgambo wa kundi la Kikurd la PKK lililouwa wanajeshi 14 wa Uturuki kwenye mpaka wa nchi hiyo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Maofisa wa jeshi la Uturuki wamesema kuwa vikosi vyao vimeingia ndani ya Ardhi ya Iraq katika mji wa Hakkari ambako ndiko kunatajwa wapiganaji wa kundi hilo wamepiga kambi wakifanya mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya vikosi vya Uturuki.
Ripoti zinasema kuwa usiku wa kuamkia leo ndege za kivita za Uturuki zimerusha mabomu katika milima ya mpakani mwa nchi hiyo ambapo kumeripotiwa vifo vya wanamgambo kadhaa bila kupatikana kwa idadi kamili ya wanamgambo waliouawa mpaka sasa.
Wachambuzi wa mambo wamekosoa hatua ya waziri mkuu Tayyip Erdogan aliyeruhusu uwepo wa ulinzi wa kiraia katika mpaka wa nchi hiyo na Iraq.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban ki Moon amelaani vikali mashambulizi hayo yanayoendelea na kuzitolea mwito serikali za Uturiki na Iraq kujadiliana ili kupata muafaka.