SYRIA-DAMASCUS

Serikali ya Syria yaeleza kufikia muafaka na Umoja wa nchi za kiarabu kumaliza machafuko nchini humo

Rais wa Syria Bashar Al-Asad
Rais wa Syria Bashar Al-Asad Reuters

Serikali ya Syria imesema tayari imefikia makubaliano na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika kumaliza machafuko ambayo yamedumu kwa miezi saba na kuchangia vifo vya waandamanaji wakati huu ambapo Kamati ya Jumuiya hiyo ikisema inasubiri kauli ya serikali.

Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya Habari vya Serikali nchini Syria vimetoa taarifa zikithibitisha kufikiwa kwa makubaliano kati ya serikali ya Rais Bashar Al Assad na Kamati ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambayo imepewa jukumu la kusaka mbinu za kumaliza machafuko hayo.

Taarifa kutoka Makao Makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yaliyopo Cairo nchini Misri zimesema wanasubiri kauli rasmi ya serikali ya Syria katika kuchukua hatua za kumaliza mgogoro uliopo unaotokana na shinikizo la kuwepo mabadiliko ya kisiasa.

Makubaliano hayo yanakuja ikiwa zimepita siku chache ambapo viongozi wa Umoja wa nchi za Kiarabu walifanya ziara nchini humo kukutana na rais Assad ambapo pamoja na mambo mengine walizungumza namna ya kumaliza umwagaji damu unaoendelea kufanywa na polisi dhidi ya raia.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa hatua hiyo ya Syria kama wataitekeleza basi huenda ikamaliza mzozo ulioppo nchini humo licha ya kuwa hautamalizika moja kwa moja mpaka pale Rais Assad atakapong'atuka madarakani.

Wakati huohuo kumeripotiwa mashambulizi dhidi ya raia katika miji kadhaa nchini humo ikiwemo miji ya Homs na Damascus ambako kumeripotiwa polisi kufanya uvamizi dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali.