ISRAEL-PALESTINA

Waziri mkuu wa Israel aagiza ujenzi wa makazi mapya katika ukanda wa Jerusalem

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu Reuters

Waziri Mkuu wa Israel Benyamin Netanyahu ameagiza ujenzi wa makazi mapya elfu mbili ya Wayahudi katika eneo la Mashariki mwa Jerusalem eneo ambalo limekuwa likitajwa na Palestina kuwa Mji Mkuu wa Taifa jipya.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu unakuja baada ya Mamlaka ya Palestina kufanikiwa kupata uanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kitu ambacho kinatajwa huenda kikaongeza uaduai baina yake na Israel.

Waziri Mkuu Netanyahu amesema kwenye taarifa yake kuwa ujenzi huo mpya wa makazi anaamini ni sehemu tu ya mkakati wa kupatikana kwa amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kauli hiyo ya waziri mkuu Netanyahu inaelezwa kuwa imetokana na kuchukizwa na hatua ya wajumbe wa UNESCO kupiga kura kuikubali rasmi nchi ya Palestina kuwa mwanachama wake wa kudumu katika shirika hilo.

Kiongozi wa zamani wa Palestina aliyekuwa akisimamia mgogoro huo Saeb Erakat, amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kisiasa zaidi na kwamba itakwamisha juhudi za kupatikana kwa suluhu katika eneo hilo.