SYRIA-DAMASCUS

Machafuko zaidi yaripotiwa nchini Syria licha ya serikali kutangaza kukubali mpango wa kuondoa majeshi katika mitaa

Waandamanaji wanaoipinga serikali katika mji wa Homs nchini Syria
Waandamanaji wanaoipinga serikali katika mji wa Homs nchini Syria Reuters

Vikosi vya Syria vikitumia vifaru na zana nyingine za kivita vimewaua raia ishirini na kuwakamata wengine ikiwa ni siku ambayo serikali ya Damascus iliahidi kuondoa majeshi yake kuridhia mpango wa Jumuiya ya Kiarabu katika kumaliza umwagaji damu uliodumu kwa miezi zaidi ya saba.

Matangazo ya kibiashara

Wanaharakati wamethibitisha kutekelezwa kwa mauaji hayo dhidi ya waandamanaji ambao wameendelea kuvamia mitaani na kushinikiza kuondoka madarakani kwa serikali ya Rais Bashar Al Assad ambayo wanaamini imezuia demokrasia ya kweli.

Mauaji haya yamesindikizwa na kauli ya serikali ya Marekani kupitia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Victoria Nuland ambaye amesema Syria itaendelea kutengwa na Jumuiya ya Kimataifa iwapo haitotekeleza mapendekezo ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Wanaharakati nchini humo wameripoti kuwasilisha taarifa yao kwa katibu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu kuelezea wasiwasi wao kuhusu utekelezwaji wa kile ambacho viongozi wa umoja huo walikubaliana na serikali ya Syria.

Kumekuwa na maandamano ya nchi nzima katika miji mbalimbali nchini Syria licha ya serikali siku ya jumatano kutangaza kuwa imeridhia makubaliano ya kusaka suluhu ya kudumu yaliyopendekezwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu.