Syria

Syria yapuuza tishio la kufutiwa uanachama na nchi za kiarabu

REUTERS/Ali Jarekji

Serikali ya Syria imesema kuwa kitendo cha kutaka kuifuta uanachama nchi hiyo katika jumuiya ya nchi za kiarabu ni kinyume na sheria za jumuiya hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem amepuuza na kuitumbilia mbali hatua hiyo ya nchi za kiarabu na kusema kuwa hatua hiyo ni hatari kwa ustawi wa Syria na nchi za kiarabu.

Matangazo ya kibiashara

Walid al-Muallem amesema kuwa ni kinyume na sheria lakini anaamini kuwa hali hiyo na hatua zinazotaka kuchukuiliwa na nchi za kiarabu zinatokana na shinikizo la Marekani.

Amesema kuwa Syria haitatishwa na hatua ya kufutiwa uanachama kwa kuwa iko katika hali ambayo ni imara na jitihada zote za kutaka kuidhoofisha nchi hiyo kamwe hazitafanikiwa.

Kauli ya Syria imekuja huku mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Ulaya wakiwa wamekutana nchini Ubelgiji na tayari wameshakubaliana katika mpango wa awali wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Hata hivyo vikwazo vya EU vitalenga katika kuwabana zaidi watu binafsi wanaojihusisha na mauaji ya raia waandamanaji wanaotaka Rais wa nchi hiyo Bashar Al-Assad aondoke madarakani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Alain Juppe amesema wakati umefika sasa kwa jumuiya kimataifa kuongeza nguvu za kuwalinda raia na amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu hilo kuanzia sasa.