ISRAELI

Fidel Castro aonya Israeli kuishambulia Iran

Reuters

Aliyekuwa rais wa Cuba Fidel Castro, amesema shambulio lolote la Israeli dhidi ya Iran huenda likaleta likazua vita baina nchi hizo mbili kama njia za kutafuta suluhu ya mgogoro hazitapatikana kwa wakati.

Matangazo ya kibiashara

Halikadhalika Fidel Castro amesema kuwa athari za mgogoro huo zitaleta sintofahamu kwa dunia nzima ukiachilia mbali athari zitakazolikumba nchi za Mashariki ya Kati.

Rais huyo wa zamani ambaye alimwachia mdogo wake mamlaka, takriban miaka mitano iliyopita kutokana na tatizo la kiafya, amesisitiza kuwa kitendo cha Israeli kutaka kuishambulia Iran ni cha hatari kwa dunia nzima.

Siku za hivi Karibuni Israeli iliionya Iran juu ya uwezekano wa kutekeleza mashambulio ya kijeshi dhidi yake huku kukiwa na hofu ya mashambulio zaidi baada ya kutolewa kwa ripoti ya waangalizi wa maswala ya Nyuklia kutoka shirika la kimataifa la nguvu za atomiki lililokuwa likishutumu Tehran kutengeneza silaha za Nyuklia.

Castro ameonya ripoti ya shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki, IAEA kuwa itaisababishia dunia kuingia kwenye vita ya Nyuklia.