Syria

Watu zaidi ya 70 wauawa nchini Syria

(REUTERS)

Watu wengine zaidi ya 70 wameuawa nchini Syria tangu jana kufuatia machafuko yanayoendelea nchini kufuatia maandamano ya wananchi wanaotaka Rais wa nchi hiyo Bashar Al-Assad aondoke madarakani. Waangalizi wa haki za binadamu kutoka Uingereza wamesema kuwa miongoni mwa watu waliouawa ni wananchi na wanajeshi ambao wengi wao waliuawa katika eneo la mji wa Daraa.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa umoja wa Mataifa watu zaidi ya 3,500 wameuawa mpaka sasa tangu kuanza kwa machafukoa na mapigano Machi 15, mwaka huu nchini Syria.

Hatua hiyo imekuja muda mchache baada ya nchi ya Jordan kumtaka Assad kuachia ngazi na kuondoka madarakani ili kuepusha mauaji yanayoendelea huku Umoja wa Nchi za Kiarabu, ukitishia kuifuta uanachama nchi ya Syria.

Hata hivyo Serikali ya Syria ilisema jana kuwa kitendo cha kutaka kuifuta uanachama nchi hiyo katika jumuiya ya nchi za kiarabu ni kinyume na sheria za jumuiya hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem alipuuza na kuitupilia mbali hatua hiyo ya nchi za kiarabu na kusema kuwa hatua hiyo ni hatari kwa ustawi wa Syria na nchi za kiarabu.

Walid al-Muallem alisema kuwa ni kinyume na sheria lakini anaamini kuwa hali hiyo na hatua zinazotaka kuchukuiliwa na nchi za kiarabu zinatokana na shinikizo la Marekani.

Alifahamisha kuwa Syria haitatishwa na hatua ya kufutiwa uanachama kwa kuwa iko katika hali ambayo ni imara na jitihada zote za kutaka kuidhoofisha nchi hiyo kamwe hazitafanikiwa.

Kauli ya Syria ilikuja huku mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Ulaya wakiwa wamekutana nchini Ubelgiji na tayari wameshakubaliana katika mpango wa awali wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Hata hivyo vikwazo vya EU vitalenga katika kuwabana zaidi watu binafsi wanaojihusisha na mauaji ya raia waandamanaji wanaotaka Rais wa nchi hiyo Bashar Al-Assad aondoke madarakani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Alain Juppe alisema wakati umefika sasa kwa jumuiya kimataifa kuongeza nguvu za kuwalinda raia na amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu hilo kuanzia sasa.