YEMEN

Rais wa Yemen aelekea Marekani kwa matibabu baada ya kuhutubia Taifa

Reuters

Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh ameondoka katika Mji Mkuu wa Omani, Muscat akiwa anaelekea nchini Marekani kwa ajili ya kupata matibabu afisa mmoja wa taifa hilo amethibitisha mapema jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Safari ya Rais Saleh kuelekea nchini Marekani imekuja saa kadhaa baada ya kuhutubia wananchi wa taifa hilo na kuomba radhi wale wote ambao walikumbwa na madhila wakati wa utawala wake wa miaka thelathini na tatu.

Afisa huyo wa serikali ameonekana kwenye Televisheni ya SABA akieleza Rais Saleh ameelekea Marekani kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na majeraha ambayo aliyapata wakati makazi yake yalipolipuliwa kwa bomu.

Saleh ambaye ametangaza uamuzi wa kukabidhi madaraka kwa Naibu wake aliondoka nchini Yemen usiku wa jumapili akiambatana na Mkewe pamoja na watoto wake wadogo watano kwa mujibu wa mtu ambaye yupo jirani na Kiongozi huyo.

Kiongozi huyo amenukuliwa akisema kuwa huu ni wakati wa kufungua ukurasa mpya na kuwataka wale wote ambao wamekuwa wakifanya maandamano kurejea nyumbani kuungana na familia zao badala ya kusalia barabarani.

Kwenye hotuba yake kwa Taifa aliwathibitishia anaelekea nchini Marekani kwa matibabu na pindi atakaporejea nchini Yemen atakuwa Kiongozi wa Chama Cha GPC na wala hatokuwa Rais tena kutekeleza matakwa ya Nchi za Ghuba.

Naye Msemaji wa Chama Cha GPC Abdul Hafiz Al Nahari amethibitisha safari ya Saleh nchini Marekani na amekanusha kuhusishwa na shughuli za kiserikali na badala yake amekwenda kimatibabu tu.

Saleh ametaka kuwepo kwa mapatano na kutoa wito kwa vijana wanaoendelea kuandamana kurudi nyumbani kuungana na familia zao ili kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya utawala mpya ujao.