Yemeni

Kiongozi wa Al Qaeda auawa kwenye mapigano Yemeni, wanafunzi 10 wafariki Palestina

Reuters / Stringer

Mapigano makali yanayoendelea nchini Yemen yameshuhudia Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Tarek Al Dahab akiuawa na ndugu yake katika Mji wa Al Masaneh ambako mapigano kati yao na majeshi yakiendelea.

Matangazo ya kibiashara

Mapigano hayo ambayo yamesababisha vifo vya watu wengine kumi na saba yanatajwa kujiegemeza zaidi kwenye ukabila Mkuu wa Jimbo la Bayda amenukuliwa akibainisha baada ya kutokea kifo hicho.

Licha ya Kiongozi huyo wa Mtandao wa Al Qaeda katike eneo hilo kupoteza maisha lakini mapigano hayajakoma na badala yake yemendelea kushuhudiwa huku kikubwa ambacho kinagombewa ni umiliki wa ardhi.

Katika hatua nyingine Wanafunzi kumi wamepoteza maisha na wengine zaidi ya thelathini wakijeruhiwa nchini Palestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi baada ya kutokea ajali iliyohusisha Basi la wanafunzi hao na lori lililokuwa linatoka nchini Israel.

Basi la wanafunzi likiwa na watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi sita likiwa linatokea Ramallah liligongana na lori ambalo baadaye lilipinduka na kisha kushika moto baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ametangaza siku tatu za maombolezi huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akipeleka salamu za rambirambi kufuatia kutokea kwa ajali hiyo.