Msafara wa Waangalizi wa UN washambuliwa Nchini Syria
Imechapishwa:
Msafara wa Waangalizi wa Umoja wa Mataifa UN waliopo nchini Syria umeshambuliwa na kusababisha uharibifu wa magari matatu wakati waaangalizi hao wakihudhuria mazishi ya watu ishirini wanaotajwa kuuawa na Utawala wa Rais Bashar Al Assad.
Shambulizi hilo la kujitoa mhanga limetokea katika ngome inayopinga Utawala wa Rais Assad kwa kipindi cha miezi kumi na mitano.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa UN Martin Nesirky yeye amewataka watu kuacha kushambulia Waangalizi kwani wao wapo kwa ajili ya kufanya tathmini ya machafuko yanavyotendeka.
Matukio haya yanaongeza hofu ya kufikiwa suluhu nchini Syria ambapo juhudi za Umoja wa Mataifa UN zimeendelea kukumbana na vikwazo hasa mashambulizi ya kujitoa mhanga ambayo yanaendelea kukithiri kwa sasa.
Katika hatua nyingine vikosi vya Serikali vimeshambulia kambi ya wakimbizi kusini mwa Syria hii leo na kusababisha watu watatu kuuawa, shirika la nchini humo linalosimamia maswala ya haki za Binaadam, limethibitisha.
Zaidi ya watu 12,000 wengi wao Raia wamepoteza maisha tangu kuanza kwa maandamano huku zaidi ya 900 wakiuawa hata baada ya mapendekezo ya mpatanishi wa UN Koffi Annan kuwasilishwa na kuanza kwa utekelezaji wake.