Yemeni

Watu wasiopungua 96 wauawa nchi Yemeni

RFI

Watu wasiopungua 96 wameuawa kutokana na shambulio la bomu la kujitoa mhanga lililotokea katika mji mkuu wa Sanaa nchini Yemeni wamesema maafisa wa Serikali.

Matangazo ya kibiashara

Shambulio hilo la bomu limetokea katika eneo ambalo wanajeshi walikua wakifanya mazoezi ya gwaride ambapo mtu aliyefanya shambulizi hilo alikua amevaa nguo za kijeshi alijilipua katika kundi la wanajeshi katika uwanja wa al-Sabin Square karibu na Ikulu ya Rais.

Shambulio linaelezewa kuwa ni kubwa kuwahi kutokea tangu rais Abdrabbuh Mansour Hadi, aingie madarakani mwezi Februari kufuatia wimbi la vuguvugu la kisiasa katika nchi za kiarabu.

Kundi la kigaidi la Al Qaeda limetangaza wazi kwamba limehusika na shambulio hilo ambalo limesababisha vifo hivyo huku wanaume wengi wakiangamia baada ya mtu huyo kujilipua.

Kundi la Al Qaeda limekuwa likilaumiwa kwa kuhatarisha usalama wa dunia kwa kufanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali duniani na shambulio hilo linaashiria kuwa bado Yemeni inakabiliwa tishio la usalama na mauaji.