Syria

Upinzani wa Syria waridhia kufanya mazungumzo yanayolenga kumaliza machafuko nchini humo

Upinzani nchini Syria umekubali kushiriki katika mkutano wa Kimataifa kuhusu machafuko yanayoendelea nchini huo baada ya Uingereza kuiomba kushiriki katika mazungumzo hayo.

Rais wa Syria, Bashar Al Assad
Rais wa Syria, Bashar Al Assad
Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo viongozi hao wa upinzani wamesema watashiriki tu katika mazungumzo hayo ikiwa yatafanyika nje ya jiji la Damascus.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Johh Kerry amesema ni muhimu kwa upinzani kushiriki katika mazungumzo hayo yatakayofanyika siku ya Alhamisi mjini Rome nchini Italia.

Kiongozi wa upinzani nchini Syria, Ahmed Moaz al-Khatib amesema kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa upinzani utahudhuria baada ya Kerry na Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza, William Hague kuahidi kutoa msaada maalum kwa ajili ya kuwasaidia waathirika nchini Syria.

Siku ya Jumamosi upinzani ulidai kuwa utajitoa katika mazungumzo ya mataifa kumi na moja rafiki wa Syria na kupanga kuzuru Washington na Moscow ili kupinga kile walichodai ukimya wa jumuia ya kimataifa katika kutafuta suluhu nchini humo.

Makamu wa Rais nchini Marekani Joe Biden amepokea kwa mikono miwili hatua mpya ya upinzani kufanya mazungumzo mjini Roma nchini Italia, ambapo watakutana na Kerry na kusema kuwa itakuwa fursa muhimu ya kutafuta njia ya kuwaunga mkono watu Syria.