ISRAEL

Israel yasisitiza kupinga mpango wa nyuklia wa Iran

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak, ameionya Iran kwamba, kamwe Israel haiwezi kuwaruhusu viongozi wa Iran kuendeleza mpango wake wa Nyuklia, kauli ambayo ameitoa mbele ya wajumbe Marekani na Israel kwenye mkutano wa mwaka wa kamati ya umma AIPAC. 

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak
Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak REUTERS/Michael
Matangazo ya kibiashara

Ehud amesema kuwa ni harakati za Iranikuona kuwa inafanikisha mpango wake wa nyuklia ambao ni changamoto kubwa inayoikabili Israel, eneo la ukanda huo na dunia kwa ujumla.
Mataifa yenye nguvu ambayo yamekuwa yakiongoza mazungumzo na Iran kuhusu kuachana na mpango wake wa nyuklia unaotiliwa hofu, walihitimisha mazungumzo yao juma lililopita nchini Kazakhstan baada ya kutoa mapendekezo ya kupunguza vikwazo ikiwa Tehran itaachana na uzalishaji wa madini ya uranium.

AIPAC, ambayo inajipigia debe kama mashawishi muhimu katika sera za kigeni za Marekani, pia itasikiliza hotuba ya moja kwa moja ya Benjamin Netanyahu ikifuatiwa na hotuba ya makamu wa rais wa Marekani Joe Biden.

Watu wapatao elfu 13,000 wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo la siku tatu litakalofanyika huko Washington, lakini mkutano huo umekuwa wa kimya kuliko miaka ya nyuma,bila uwepo wa Rais Barack Obama wala Rais wa Israel Shimon Peres.