SYRIA

Majadiliano juu ya kuachiwa kwa walinda amani wa UN waliotekwa Syria yaendelea

REUTERS/Muzaffar Salman

Maofisa wa Umoja wa Mataifa UN wamesema majadiliano yanaendelea kati yao na waasi wa Syria waliowateka walinda amani ishirini na moja wa UN kwenye eneo la Golan katika mpaka wa Syria na Israel. Walinda amani hao wa UN walitekwa siku ya jumatano wakituhumiwa na waasi kuwa ni kikwazo katika mapambano ya kuuangusha utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa walinda amani ya Umoja wa Mataifa Herve Ladsous amewaambia waandishi wa habari kuwa majadiliano yanaendelea na suala linaloangaliwa hivi sasa ni kuhakikisha usalama wao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito wa kuachiwa mara moja kwa Walinda amani hao na kuitaka serikali ya Syria na waasi kuheshimu haki yao na usalama.

Wakati hayo yakijiri Msemaji wa waasi amesema wataendelea kuwashikilia watu waliowateka mpaka pale vikosi vya Rais Assad vitakapoondoka katika eneo la Golan.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa watu zaidi ya elfu sabini wameripotiwa kupoteza maisha tangu kuanza kwa mapigano nchini Syria miaka miwili iliyopita.