ISRAEL

Baraza jipya la mawaziri la Israel kuapishwa jumatatu ijayo

REUTERS/Sebastian Scheiner/Pool

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wa chama cha mrengo wa kushoto pamoja na washirika wake katika serikali ya muungano toka mrengo wa kulia wamefanikiwa kutupilia mbali changamoto zao baada ya kufikia makubaliano ambayo yatashuhudia serikali mpya ijumaa hii.

Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa kiongozi wa chama cha Yesh Atid, Yair Lapid na Naftali Bennett wa Jewish Home wamelegeza msimamo wao katika suala la Naibu Waziri Mkuu, suala ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa katika kufikia muafaka wa serikali ya muungano.

Baada ya makubaliano hayo serikali mpya inatarajiwa kuwasilishwa kwa Rais Shimon Peres hapo kesho na baraza jipya la mawaziri linatarajiwa kuapishwa mbele ya bunge jumatatu ijayo masaa 48 kabla ya Rais wa Marekani Barack Obama kuzuru nchini Israel.

Wizara ya fedha na elimu inatarajiwa kuwa chini ya upande Yesh Atid ambao walinyakua viti 19 vya bunge kati ya 120 katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Upande Jewish Home wanatarajia kuongoza wizara za viwanda na biashara pamoja na ile ya makazi ambayo inahusika na ujenzi wa makazi ya Wayahudi katika eneo lenye mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Wizara ya mambo ya nje, ulinzi na mambo ya ndani zitakuwa chini ya upande wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu ambaye muungano wake wa kisiasa ulinyakua viti 31 katika uchaguzi wa wabunge.