SYRIA

Marekani na Uingereza zatilia mkazo ushirikiano wa Urusi katika kutatua mzozo wa Syria

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron www.mirrow.co.uk

Marekani na Uingereza wameendeleza shinikizo kwa Urusi ili iweze kushirikiana nao katika kuhakikisha wanapata suluhu ya mgogoro wa Syria huku msimamo wa mataifa hayo ukiwa wazi kwamba ni lazima Rais Bashar Al Assad aondoke kwanza madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Mataifa hayo yameongeza shinikizo kabla ya kufanyika kwa mkutano wa mataifa manane tajiri zaidi duniani maarufu kama G8 ambapo rais wa Marekani Barack Obama amesema lazima Assad aondoke kwanza ndiyo suluhu itapatikana.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron kwa upande wake amesema wataendelea kutoa msaada kwa wapinzani kwa kuwa wanalitambua kundi hilo kama mwakilishi halali wa wananchi.

Viongozi hao wameshindwa kuweka wazi msimamo wao iwapo watakuwa tayari kuwapatia silaha wapiganaji wa upinzani ili waweze kufanikisha vita yao ya kuiangusha serikali ya Rais Assad wanayopambana nayo kwa kipindi cha miezi ishirini na sita sasa.