ISRAEL

Israel yawaacha huru Wafungwa 26 wa Palestina

Waziri Mkuu wa Israel Benyamin Netanyhau
Waziri Mkuu wa Israel Benyamin Netanyhau REUTERS/Ronen Zvulun

Israel imewaachia huru wafungwa wa Palestina 26 hii leo huku ikiahidi kujenga makazi ya walowezi, saa kadhaa kabla ya pande hizo mbili kukutana kwa ajili ya mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana ya amani ambayo yalikuwa yamekwama kwa takriban miaka mitatu.

Matangazo ya kibiashara

Wakati Raia wa Palestina wakishangilia kufunguliwa kwa kundi la kwanza la wafungwa 104, wengi wao waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha kwa kuwa ua Raia wa Israeli, Waziri wa makazi Uri Ariel ameapa kujenga maelfu ya nyumba za walowezi katika ukingo wa magharibi.
 

Ariel amesema kuwa mwaka unaokuja wataendelea kujenga makazi mengi katika mji wa Yudea na Samaria.
 

Kauli hiyo inayoelezwa kuwa ya uchochezi imetolewa wakati ujumbe wa pande mbili ukijiandaa kufanya mazungumzo baada ya jitihada za Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kuzitaka Israel na Palestina kumaliza tofauti zao.
 

Ingawa hatua ya kufunguliwa kwa Wafungwa wa Kipalestina ilikaribishwa kwa mikono miwili na Palestina haikuweza kutuliza ghadhabu zao baada ya Israel kutangaza kuendeleza mpango wake wa kujenga makazi mapya 2,129 ya walowezi mashariki mwa Yerusalemu.
 

Mazungumzo ya kupatikana amani zilivunjika mara ya mwisho majuma kadhaa baada ya kuzinduliwa kwa makazi ya walowezi mwaka 2010.