ISRAEL

Katibu Mkuu wa UN atoa wito kwa Israel na Palestina kuepuka vitendo vitakavyodhoofisha mazungumzo ya amani

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban Ki Moon. REUTERS/Charles Platiau

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito kwa Raia wa Israel na Palestina kuondoa tofauti hasi kila mmoja alizonazo juu ya mwingine ambazo ameeleza zitaathiri jitihada za kufikia makubaliano ya amani.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza alipokutana na mjini Jerusalem na Rais wa Israel, Shimon Peres amezitaka pande zote kuepuka vitendo vitakavyoathiri mazungumzo ya amani na kuwataka kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuupa nafasi mchakato wa kufikiwa kwa amani.

Mazungumzo ya jumatano, ambayo yalikuwa matunda ya jitihada za kidiplomasia za Marekani kuzirejesha Israel na Palestina kwenye meza ya mazungumzo baada ya kukwama kwa takriban miaka mitatu, yalifunikwa na tangazo juu ya mpango wa Israeli kujenga makazi mapya ya Walowezi.
 

Wakati huu mchakato wa kupatikana amani kati ya mataifa hayo mawili ukipamba moto, Israel ilitangaza mpango wa kujenga zaidi ya Makazi 2,000 mashariki mwa Jerusalem na maeneo mengine ya ukingo wa Magharibi hatua ambayo imewaghadhabisha Maafisa wa Palestina.
 

Ban hao jana alikosoa mpango huo wa Israeli katika mkutano kati yake na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas katika mji wa Ramallah lililo ukingo wa magharibi.
 

Ban alionesha kufadhaishwa na mpango huo wa Israel akisema kuwa mipango hiyo inavunja uaminifu wa Raia wa Palestina juu ya umakini na nia thabiti ya Israel katika kufikia makubaliano ya amani, hatua aliyosema kuwa inafanya suluhu la mzozo wa pande hizo mbili kuwa kushindikana kufikiwa.
 

Lakini Waziri Mkuu wa Israel, Benjamini Netanyahu alikwepa kuzungumzia suala la Makazi akisema kuwa Chanzo cha mgogoro kati ya israel na Palestina ni kukataa kuitambua Palestina kama taifa.
 

Amesisitiza kuwa mgogoro huo hauhusiani na makazi na kuwa hilo ni suala ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi na si sababu ya mzozo kati ya nchi hizo.