Lebanon-shambulizi

Watu 27 wapoteza maisha nchini Lebanon katika milipuko miwili iliotokea katika jiji la Tripoli

Shambulio la bomu huko Lebanon
Shambulio la bomu huko Lebanon

Watu ishirini na saba wamepoteza maisha nchini Lebanon huku wengine mia tatu na hamsini na wawili wakijeruhiwa baada ya kutokea milipuko miwili mikubwa katika Jiji la Tripoli lililopo Kaskazini mwa Taifa hilo. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Afya nchini Lebanon Ali Hassan Khalil ndiye ametoa takwimu hizo na kuthibitisha watu hao kupoteza maisha kwenye milipuko hiyo miwili iliyotikisa Taifa hilo na hakuna Kundi lolote ambalo limetangaza kuhusika kwa namna yoyote kupanga au kutekeleza shambulizi hilo baya.

Shambulizi la kwanza lilitekelezwa katikati ya Jiji la Tripoli karibu kabisa na makazi ya Waziri Mkuu ambaye anamaliza muda wake Najib Mikati na taarifa zinasema wakati shambulizi hilo likifanyika yeye hakuwepo.

Duru za kiusalama nchini Lebanon zinaweka bayana shambulizi la pili lilitekelezwa katika mji wenye waumini wengi wa Kisunni na jirani kabisa na nyumba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi wa zamani Ashraf Rifi.

Mashambulizi haya yanayohofiwa kuwa ya kigaidi yanakuja ikiwa ni siku mbili pekee baada ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Jean Kahwaji kusema wameunda kikosi maalum ambacho kitaendesha vita dhidi ya magaidi.