SYRIA

Msafara wa mwisho wa waasi waondoka mjini Homs

Vikosi vya rais Assad vikisimamia zoezi la kuondoka kwa waasi  katika eneo la Old City mjini Homs
Vikosi vya rais Assad vikisimamia zoezi la kuondoka kwa waasi katika eneo la Old City mjini Homs REUTERS/Ghassan Najjar

Serikali ya Syria leo Jumamosi inafurahia ishara ya ushindi wakati huu raia wanaanza kurejea katika mji wa Old City jijini Homs baada ya waasi wa mwisho kuondoka chini ya mpango wa uokoaji. 

Matangazo ya kibiashara

Kuondoka kwa waasi kumekamilika jana Ijumaa, na kuwaacha waasi katika wilaya moja nje kidogo ya mji wa kati, ambao wakati mmoja uliitwa mji mkuu wa mapinduzi dhidi ya Rais Bashar al-Assad.

Wakati askari wakiingia mjini humo kusafisha na kuondoa mabomu, mamia ya raia walianza kurudi kuona kile kilichosalia katika nyumba zao huko Hamidiyeh, wilaya ya Kikristo katika mji huo ambayo umekuwa chini ya mashambulizi ya mabomu karibu kila siku wakati wa miaka miwili ya mkwamo.

Wengi wa wakaazi wamekumbwa na mshtuko na kutokwa na machozi wakati wakipanda juu ya mabaki ya majengo kukagua uharibifu uliofanywa.

Msafara wa mwisho wa waasi umeendoka baada ya kucheleweshwa kwa muda mrefu huku shutuma za kuchelewa huko zikielekezwa kwa wapiganaji wa Kaskazini mwa Syria kuzuia msafara wa msaada uliokuwa unapelekwa kwenye miji miwili inayounga mkono serikali inayokabiliwa na wapiganaji wa upinzani kwenye jimbo la Aleppo.