SYRIA

Wananchi wa Syria wapiga kura kuchagua rais, huku upinzani ukisusa kushiriki

Wananchi wa Syria wakipiga kura wakiwa na picha za rais wao, Bashar al-Assad.
Wananchi wa Syria wakipiga kura wakiwa na picha za rais wao, Bashar al-Assad. REUTERS

Wananchi wa Syria hii leo wanapiga kura kwenye uchaguzi wa rais, uchaguzi ambao umesusiwa na upinzani nchini humo pamoja na mataifa ya magharibi ambayo yalitaka utawala wa rais Bashar al-Assad kutofanya uchaguzi huo. 

Matangazo ya kibiashara

Saa chache baada ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa mamia ya wananchi walionekana kwenye misururu wakisubiri kuanza kwa zoezi la kupiga kura, kwenye uchaguzi ambao wengi wanampa nafasi rais Assad kuendelea kusalia madarakani.

Wananchi wa Syria wakipiga kura kwenye Ubalozi wa Jordan
Wananchi wa Syria wakipiga kura kwenye Ubalozi wa Jordan REUTERS

Hata hivyo uchaguzi huu unafanyika kwenye maeneo ambayo vSerikali inaumiliki huku kwenye maeneo yanayokaliwa na waasi zoezi hilo halitafanyika kwa sasa kutokana na sababu za kiusalama na waasi wa nchi hiyo kuwazuia wananchi kushiriki.

Wachambuzi wa mambo na wanasiasa wa nchi ya magharibi wameonya kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huu ambao wanadai hata kama utamalizika kwa amani kwenye maeneo mengi ya nchi, uteuzi wa rais Assad utachochea vurugu zaidi kwenye taifa hili.

Rais wa baraza la upinzani wa Syria, Ahmad Jarba
Rais wa baraza la upinzani wa Syria, Ahmad Jarba REUTERS/Jamal Saidi

Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanyika kwenye maeneo mengi ambayo Serikali inayamiliki, wananchi wengi wameonesha kuwa bado wanamuunga mkono rais Assad licha ya ukosolewaji mkubwa inaoipata Serikali yake.

Raia wa Syria wanaoishi nje ya taifa la Syria wao watapiga kura kwenye balozi za nchi hiyo.

Zoezi hili linafanyika wakati huu ambapo hapo jana waasi wa Syria walitekeleza shambulizi la kujitoa muhanga kwenye mji wa Homs na kuua watu zaidi ya kumi na kujeruhi wengine kadhaa.

REUTERS/Khaled al-Hariri

Kiongozi wa baraza la muungano wa waasi wa Syria, Ahmad Jarba ametoa wito kwa wananchi wa taifa hilo kukaa nyumbani na kutoshiriki kwenye uchaguzi huu ambao wao wamesema hawautambui huku wanaharakati wakisema ni uchaguzi unaohalalisha umwagikaji damu nchini Syria.

Wizara ya mambo ya ndani ya Syria imesema kuwa zaidi ya wananchi milioni 15 wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi, uchaguzi ambao ni kwanza kuelezwa kuwa wa kidemokrasia katika kipindi cha miaka 50.