Dr Abdullah anusurika kifo kwenye shambulio la bomu mjini Kabul
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa nchini Afghanistan, Abdullah Abdullah amenusurika kuuawa kwenye shambulio la bomu la kujitoa muhanga lililolenga msafara wake mjini Kabul.
Shambulio hili limetekelezwa wakati huu wananchi wa Afghanistan wakijiandaa kushiriki kwenye duru ya pili ya uchaguzi mkuu.
Akizungumza na wafuasi wake kwenye mkutano mwingine wa hadhara saa chache baada ya msafara wake kushambuliwa, Abdullah anasema "dakika chache zilizopita wakati tulipomaliza mkutano wetu wa kampeni tulishambuliwa kwa bomu". Alisema Abdullah Abdullah.
Polisi mjini Kabul wamethibitisha kutokea kwa shambulio hili na kuongeza kuwa mtu aliyejifanya kuwepo kwenye msafara wa kampeni za Abdullah akitumia gari, alijilipua jirani kabisa na gari alilokuwemo mgombea huyo.
Polisi wanasema kuwa watu wanne ndio wameripotiwa kupoteza maisha kwenye shambulio hili la kwanza kumlenga mmoja wa watu wanaowania kiti cha urais nchini humo na kwamba watu zaidi ya 16 wamejeruhiwa.
Shambulio hili linatekelezwa wakati huu taifa hilo likijiandaa na uchaguzi wa raundi ya pili, uliopangwa kufanyika tarehe 14 ya mwezi June mwaka huu, uchaguzi ambao wanamgambo wa Taliban wametishia kuvuruga zoezi lote.
Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika kwenye shambulio hili, ingawa taarofa za awali zinaeleza kuwa huenda wakawa ni wapiganaji wa kundi laTaliban nchini humo.
Abdullah ambaye hakufikisha asilimia 50 ya idadi ya kura zinazohitajika kumuwezesha kushinda uchaguzi huo, anatarajiwa kupambana na mwenzake, Ashraf Ghani aliyewahi kuwa mshauri wa uchumi kwenye benki kuu ya dunia.