IRAQ

Wapiganaji wa Kisunni nchini Iraq wadhibiti kampuni ya mafuta

Wapiganaji wa Kisunni nchini Iraq
Wapiganaji wa Kisunni nchini Iraq

Wapiganaji wa Kisunni nchini Iraq wanasema wanadhibiti kikamilifu Kampuni kubwa ya kuzalisha mafuta katika mji wa Baiji Kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kumekuwa na makabiliano makali kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji hao katika siku za hivi karibuni.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry yupo katika mji wa Irbil Kaskazini mwa nchi hiyo kwa siku ya pili leo kuongoza mazungumzo kati ya viongozi wa nchi hiyo kujaribu kupata suluhu la kudumu.

Wapiganaji hao wa Kisunni wamefanikiwa kuchukua miji ya Kaskazini na Magharibi mwa nchi hiyo na mji wa pili kwa ukubwa wa Mosul, yakiwemo maeneo karibu na nchi za Syria na Jordan.

Aidha, wapiganaji hao wanasema baada ya kuchukua kampuni hiyo ya mafuta, sasa wataikabidhi kwa kabila katika eneo hilo ili kuiongoza wakati huu wanapoendelea na mapambano ya kuuchukua jiji Kuu la Baghdad.

Kampuni ya mafuta ya IRAQ
Kampuni ya mafuta ya IRAQ REUTERS/Thaier al-Sudani/Files

Kazi kubwa ya Kerry nchini Iraq ni kujaribu kuishawishi serikali ya Kishia inayoongozwa na Waziri Mkuu Nuri al- Maliki kufanya kazi na kila mmoja kwa lengo la kuliunganisha taifa hilo ambalo limekuwa vitani kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Wapiganaji hao wanasema lengo lao ya kupambana na serikali ni kuiondoa madarakani, na tayari serikali ya Waziri Mkuu al-Maliki imekiri kuonekana kulemewa na imeomba msaada kwa serikali ya Marekani kuisaidia kupambana na wapiganaji hao kwa kutuma ndege zao zisizokuwa na rubani.

Marekani imesema kuwa itatuma wanajeshi wake 300 kuwashauria wanajeshi wa Iraq na wala haitatuma wanajeshi wake wa ardhini kupambana na wapiganaji hao.