ONU-SYRIE-Upatanishi-Siasa

Msuluhishi mpya katika mzozo wa Syria apatikana

Staffan de Mistura ameteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa msuluhishi wa mzozo wa Syria.
Staffan de Mistura ameteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa msuluhishi wa mzozo wa Syria. (Photo : AFP)

Staffan de Mistura raia wa Italia na Sweden ameteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa msuluhishi wa mzozo wa Syria, kuchukua nafasi ya Lakhdar Brahimi raia wa Algeria aliyejiuzulu mwezi wa tano.

Matangazo ya kibiashara

Uteuzi huo wa Staffan de Mistura umethibitishwa na mataifa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na ulikua unatazamiwa kutangazwa rasmi hapo jumatano wiki hii na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

Staffan de Mistura anachukua na fasi ya mtangulizi wake Lakhdar Brahimi aliejiuzulu mwezi Mei mwaka 2014.
Staffan de Mistura anachukua na fasi ya mtangulizi wake Lakhdar Brahimi aliejiuzulu mwezi Mei mwaka 2014. AFP PHOTO / MASSOUD HOSSAINI

De Mistura atakuwa na kibarua cha kutafuta suluhu ya kisiasa nchini humo.

De Mistura mwenye umri wa miaka 67, amewahi kuwa naibu waziri wa Mambo ya nje wa Italia na kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya miaka 30.

Ban Amesema kuna ulazima pande husika katika mzozo wa Syria zihakikishe uteuzi wa De Mistura, na zoezi hili litachukua muda kwa kukutana na pande zote hizo ili zikubalishe kwa pamoja kuwa zimeunga mkono uteuzi huo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon. REUTERS/Michael Kooren

Kwa mujibu wa mjumbe mmoja wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, de Mistura atawakilisha Umoja wa Mataifa, lakini Brahimi alikua mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Mataifa ya Kiarabu. De Mistura atakua na naibu wake atakaye wakilisha Umoja wa Mataifa ya Kiarabu, ambaye ambaye bado hajateuliwa.

Lakhdar Brahimi alijiuzulu mwezi Mei, baada ya miaka miwili akijitahidi kupatanisha pande mbili husika katika mzozo ambao umesababisha vifo vya watu 160.000 tangu mwezi Machi mwaka 2011. Brahimi aliandaa mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana kati ya serikali ya Syria na upinzani, laikini mazungumzo hayo yaligonga mwamba.

Mtangulizi wake, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Matifa, Kofi Annan, alijiuzulu miezi sta baada ya uteuzi wake mwaka 2012.

Hayo yakijiri, upinzani nchini Syria ambao unaungwa mkono na mataifa ya magharibi, Saudi Arabia na Qatar, umemteua hapo jumatano wiki hii katika mji mkuu wa Uturuki, Istanbul, Hadi El-Bahra kuwa kiongozi mpya wa upinzani huo kwa lengo la kukomesha mgawanyiko unaoendelea kujitokeza katika upinzani dhidi ya utawala wa Bashar Al assad.

Hadi el-Bahra, ambaye anaungwa mkono na mtangulizi wake, Ahmad Jarba na Saudi Arabia, ambako anaishi, ameteuliwa katika mkutano uliyoandaliwa mbali kidogo na mji wa Istanbul.