ISRAELI-PALESTINA-HAMAS

Israel na Hamas zavunja makubaliano ya kusitisha mapigano kwa saa 72

Mapigano yakiendelea huko Gaza
Mapigano yakiendelea huko Gaza REUTERS/Mohamad Torokman

Takribani wapalestina 107 wameuawa na askari wa Israel hajulikani alipo ikihofiwa kuwa ametekwa nyara, baada ya machafuko mapya kuzuka na kuenea katika eneo la ukanda wa Gaza leo Jumamosi baada ya Israel na Hamas kushindwa kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano. 

Matangazo ya kibiashara

Mashambulizi yamendelea usiku kucha na kusababisha vifo vya wapalestina takribani 35 katika mji wa Rafah peke yake huko Gaza, katika mfululizo wa mashambulizi yaangani yaliyofanywa na Israel tangu usiku wa manane jana Ijumaa.

Rais wa Marekani Barack Obama ametoa wito wa kuachiwa bila masharti kwa askari wa Israel Luteni Hadar Goldin mwenye umri wa miaka 23 ambaye hajulikani alipo, na kuongeza kuwa jitihada zaidi lazima zifanywe ili kuwalinda raia wa Gaza.

Mapigano makali hapo jana Ijumaa na mapema leo Jumamosi,ambayo yametokea baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku tatu,yamesababisha kuvunjika kwa makubaliano hayo saa kadhaa baada ya kuanza kutekelezwa ambapo kundi la Hamas linaishutumu Israel kwa kuvunja makubaliano hayo ya muda mfupi huku Israel ikisema ilikuwa ikijibu mashambulizi ya roketi yanayofanywa na Hamas.