IRAQ-MAREKANI-ISIL-Usalama

Iraq: UN yatuma tume ya uchunguzi kuhusu uhalifu unaotekelezwa na wapiganaji wa kiislam

Mpiganaji wa kiislam akipiga doria kwenye moja ya randabauti za mji wa Mossoul, Juni 11 mwaka 2014.
Mpiganaji wa kiislam akipiga doria kwenye moja ya randabauti za mji wa Mossoul, Juni 11 mwaka 2014. REUTERS/Stringer

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limechukua uamzi wa kutuma tume ya kuchunguza kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kutekelezwa na wapiganaji wa kiislam nchini Iraq. Wachunguzi 11 wanatazamiwa hivi karibuni kuwasili nchini Iraq.

Matangazo ya kibiashara

Pendekezo la kuanzisha uchunguzi kuhusu uhalifu huo umepigiwa kura na wajumbe wote wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake maalumu. Wachunguzi hao watawasalisha nyaraka zao mbele ya baraza hilo katikati ya mwezi wa Septemba mjini Geneva.

Kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kimeitishwa jumatatu wiki hii baada ya kuombwa na serikali ya Iraq na wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Wajumbe katika kikao hicho wamelani mauaji yanayotekelezwa na wapiganaji wa kiislam, na kusema kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Baraza hilo limetoa wito wa kusitisha haraka iwezekanavyo ufadhili kwa makundi ya kigaidi. Baadhi ya wajumbe wakiona kwamba makundi hayo ya wapiganaji wa kiislam kuwa siyo tishio tu kwa ukanda, bali ni tishio kwa ulimwengu mzima.

Umoja wa Mataifa umelituhumu taifa la kiislam kutekeleza uhalifu wa kivita, ukiukwaji wa haki za binadamu na kupandikiza chuki ya ukabila na dini. Hata hivo Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati ili uhalifu huo ukomeshwe.

■ Tume ya Umoja wa Mataifa yatuhumu vikali jeshi la Iraq

Kwa mujibu wa naibu kamishna mkuu wa Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, flavia Pansieri, hata kama wajumbe na wapiganaji wa taifa la kiislam wamehusika na mauaji ya raia wasiyokua na hatia, vilevile jeshi la Iraq liliwafanyia raia vitendo viovu, hususan kuwafanyia vipigo na maovu mengine.