YEMEN

Shirika la Msalaba mwekundu laomba mashambulizi ya angaa nchini Yemen kusitishwa kwa muda

Athari ya mapigano nchini Yemen
Athari ya mapigano nchini Yemen REUTERS/Mohamed al-Sayaghi

Shirika la msalaba mwekundi linaomba mashambulizi ya angaa yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Kihouthi katika maeneo mbalimbali nchini Yemen yasitishwe kwa muda wa saa 24 ili kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa.

Matangazo ya kibiashara

Mashambulizi hayo yanaendelea hasa jijini Sanaa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili pendekezo la Urusi la kutaka kuwepo kwa mapumziko katika mashambulizi hayo ya angaa.

Marie-Claire Feghali msemaji wa Shirika la Msalaba mwekundu anasema mapigano yanyoendelea jijini Sanaa na Aden yanastahili kusitishwa kwa muda ili kushughulikia hali ya kibinadamu katika miji hiyo.

Wakaaazi wa Sanaa wanakosa huduma muhimu kama chakula na matibabu ya afya kutokana na mapigano hayo yanayoendelea.

Takriban watu 44, ikiwa ni pamoja na raia wa kawaida 18, wameuawa katika mapigano yaliyotokea Alhamisi wiki hii katika mji wa Aden.

Ripoti zinasema kuwa huenda Ikulu ya rais katika mji wa Aden iko mikononi mwa waasi, kwa mujibu wa mashahidi na Ofisa mmoja wa wizara ya ulinzi.
Hata hivyo, hali bado ni tete.

Waasi wa Kishia wanasadikiwa kuwa wameiteka Ikulu ya rais mjini Aden.

Kwa mujibu wa shahidi aliyehojiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP amesema,” Mamia ya waasi na washirika wao waliwasili Alhamisi wiki hii wakiwa katika magari yao ya kijeshi pamoja na vifaru waliingia katika Ikulu ya rais Al-Maashiq”.

Alhamisi jioni Aprili 2, afisaa mmoja wa wizara ya ulinzi alithibitisha kwamba Ikulu ya rais katika mji wa Aden iko mikononi mwa waasi, akibaini kwamba Ikulu hiyo ilikua chini ya ulinzi “ wa vikosi maalumu, vinavyomtii Ali Abdallah Saleh”, rais wa zamani aliyekabidhi madaraka mwaka 2012, baada ya mwaka mmoja wa maandamano ya raia.

Uharibifu nchini Yemen
Uharibifu nchini Yemen REUTERS/Khaled Abdullah

Kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi, wapiganaji wa kundi la waasi wa Kishia kutoka jamii ya Houthi, wameuawa katika mapigano hayo ya Alhamisi wiki hii.

Ahmed Waashuri, msemaji wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita dhidi ya waasi, amesema kwamba hali ya usalama katika mji wa Aden " imeimarika".

" Wanamgambo wa Kishia kutoka jamii ya Houthi hawana udhibiti wa jengo lolote la serikali katika mji huo", ameongeza Ahmed Waashuri, bila hata hivyo hasa kutaja ikulu ya rais.