YEMEN-SAUDI ARABIA-HOUTHI-VITA-SIASA

Yemen: msaada wa kibinadamu wawasili kwa kiwango kidogo

Shirika la Afya Duniani (WHO) imeongeza idadi ya waathirika wa machafuko Yemen kufikia watu 643 waliuawa na 2,226 waliojeruhiwa tangu tarehe 19 Machi mwaka 2015.
Shirika la Afya Duniani (WHO) imeongeza idadi ya waathirika wa machafuko Yemen kufikia watu 643 waliuawa na 2,226 waliojeruhiwa tangu tarehe 19 Machi mwaka 2015. REUTERS/Mohamed al-Sayaghi

Mapigano yameendelea kurindima katika mji wa pili wa Yemen wa Aden, kusini mwa nchi hiyo kati ya wafuasi na wapinzani wa rais Abd Rabbo Hadi Mansour, ambaye alikimbilia ukimbizini nchini Saudi Arabia.

Matangazo ya kibiashara

Takriban watu 22 waliuawa Jumatano wiki hii katika mashambulizi yaliyoendeshwa na waasi wa Houthi, na wengine 70 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida.

Meli za kwanza zinazobeba msaada wa kiutu zimewasili katika mji wenye bandari wa Aden. Hata hivyo msaada huo unaonekana kutowatosheleza walengwa.

Meli moja kutoka Djibouti imeweza kupakua tani 2.5 za dawa kwa ajili ya hospitali ya Aden. Huu ni msaada wa kwanza wa kibinadamu kuwasili katika mji wa Aden tangu kuanza kwa mashambulizi yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi  nchini Yemen.

" Msaada huo ni pamoja na dawa na vifaa vingine vinavyotumiwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa na majeruhi", amesema Dk Abdullah Radman, msemaji wa Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka katika mji wa Aden.

Dk Ramdan amesema kwamba msaada huo hautoshi ikilinganishwa na idadi ya waathirika.

" Ndani ya kipindi cha siku kumi, tumepokea zaidi ya majeruhi 660. Tunahitaji msaada zaidi. Tunasubiri siku mbili zijazo tani kumi ya dawa, ambazo zitawasili kwa meli au kwa ndege", ameongeza Dk Ramdan.


" Hali ya kibinadamu ni mbaya katika mji wa Aden tangu kuanza kwa machafuko na hali hiyo inazidi kuwa mbaya"
, amethibitisha kwa upande wake Marie-Claire Frali, msemaji wa shirika la msalaba mwekundu duniani ICRC.

" Sehemu kubwa ya mji huo imezingirwa. Njia ya majini na angani zimefungwa. Na kutokana na mapigano yanayoendelea ni vigumu kutumia barabara. Wakaazi wa mji huo hawawezi hata kutoka nje ya nyumba zao na kwenda kununua chakula au maji. Hata hivyo, uhaba wa mafuta unaripotiwa katika mji wa Aden. Miili ya watu waliouawa imetapakaa mji mzima, huku ndugu wa marehemu wakishindwa kuchukua miili ya ndugu zao kwa ajili mazishi", ameongoza Frali.

Wengi mwa wakimbizi kutoka Yemen wamekimbilia Djibouti, na wengine nchini Saudi arabia na Somalia.

Hayo yakijiri, Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya nje, John Kerry ameionya Iran kwa uamzi wake wa kuwaunga mkono waasi, baada ya nchi hiyo kutuma mawari zake mbili katika ghuba ya Aden.