YEMEN-Al QAEDA-HOUTHI-VITA-SIASA

Yemen: Al Qaeda yadhibiti uwanja wa ndege na eneo la mafuta

Wapiganaji wa vikosi vya kikabila katika mji wa Shihr kwenye umbali wa kilomita hamsini kutoka Moukalla, Aprili 4mwaka 2015.
Wapiganaji wa vikosi vya kikabila katika mji wa Shihr kwenye umbali wa kilomita hamsini kutoka Moukalla, Aprili 4mwaka 2015. REUTERS/Omer Arm

Mtandao wa Al-Qaeda umedhibiti Alhamisi Aprili 16 uwanja wa ndege wa Moukalla, mji mkuu wa jimbo la Hadramout kusini mashariki mwa Yemen.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo, wapiganaji wa kikabila wamechukua udhibiti wa eneo muhimu la mafuta kilomita 50 mashariki ya Moukalla. Mapigano yanaendelea kurindima nchini Yemen tangu Machi 26, siku yalipoanza mashambulizi ya anga ya muungano wa Kiarabu unaoongozwa na Suadi Arabia.

Uwanja wa ndege wa Moukalla na eneo la mafuta la Al-Chehr vimedhibitiwa na Al Qaeda bila ya umwagaji damu, baada ya kuondoka kwa vikosi vya kijeshi viliyokua vikitoa ulinzi katika maeneo hayo. Moukalla, mji wenye wakaazi 200,000 kwa sasa unadhibitiwa na kundi la Ansar al-Sharia, tawi la al-Qaeda.

Kambi ya jeshi ya 27 inayomtii Rais Hadi aliyekimbilia Saudi Arabia, ambayo inapatikana mashariki mwa Moukalla ndio pekee haijadhibitiwa na Al-Qaeda.

Kuhusu kudhibitiwa kwa eneo la mafuta la Al-Chehr na vikosi vya kikabila, ni muendelezo wa ushindi, uliyotangazwa Jumanne Aprili 14. Eneo la mafuta la Al-Chehr ni moja maeneo muhimu katika kanda wa Mashariki ya Kati. Uwezo wake wa kuuza mafuta nje ni kati ya mapipa 120 na 140,000 (ya mafuta yasiyosafishwa) kwa siku.

Kwa upande mwingine, Alhamisi Aprili 16 mapigano mapya yameripotiwa katika mji wa Taez, mji mkubwa wa tatu, kwa mujibu wa wakazi wa mji huo. Mapigano makali yaliyofanyika katika mji huo ambapo waasi na washirika wao, wanajeshi waaminifu kwa Rais wa zamani Saleh, wamekua wakijaribu kuwaondoa wanajeshi wanaomuunga mkono rais Abd Rabbo mansour Hadi, kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi na mashahidi. Hatua ambayo inaweza kusababisha hali ya kibinadamu kuzidi kuwa ngumu zaidi.