Syria: watu zaidi ya 60 wauawa katika mashambulizi ya jeshi la serikali
Kwa uchache watu 82, wengi wao wakiwa raia wa kawaida, wameuawa Jumapili Agosti 16 katika mashambulizi ya angani ya jeshi la utawala wa Bashar al-Assad karibu na mji wa Damascus, siku ambayo mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu amekua akikutana na maafisa katika mji mkuu wa Syria.
Imechapishwa:
Ndege za kijeshi zimeendesha mashambulizi katika mji wa Duma, mji unaoshikiliwa na waasi ambao unapatikana kwenye umbali wa kilomita 13 Kaskazini Mashariki mwa Damascus, na karibu kila siku mji huo umekua ukishuhudiwa mashambulizi ambayo yamekua yakisababisha vifo vingi, mashambulizi ambayo yamekua yakiendeshwa na jeshi la utawala wa Bashar al Assad dhidi ya waasi.
" Jeshi la serikali limeendesha mashambulizi mara sita katika soko lenye watu wengi katikati mwa mji wa Duma na mara nne pembezoni mwa eneo hilo. Watu 82 wameuawa katika mashambulizi hayo na zaidi ya 250 wamejeruhiwa ", Rami Abdel Rahman, mkurugenzi wa shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH), ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP. OSDH ni shirika lisilo la kiserikali ambalo lina mtandao mpana wa vyanzo nchini Syria.
" Baada ya ya shambulizi la kwanza, watu walikusanyika sehemu moja na mashambulizi mengine yalifuatiwa ", Rami Abdel Rahman amesema, huku akiongeza kuwa majeruhi wengi walikuwa katika hali mbaya.
Kwa mujibu wa Rami Abdel Rahman, wengi miongoni mwa waliouawa au kujeruhiwa ni raia wa kawaida.
" Haya ni mauaji ya makusudi ", amebaini Abdel Rahman.
" Assad ametekeleza mauaji mapya katika mji wa Duma, akilenga soko lenye watu wengi ", muungano wa vyama vya upinzani nchini Syria uishio uhamishoni umelaani kwenye Twitter.
Majumba mengi yamebomoka kutokana na mashambulizi hayo, huku watu wengi wakipoteza mali zao.
-'Uhalifu wa kivita' -
Jumatano Agosti 12, ripoti ya shirika la kimataifa la Haki za binadamu, Amnesty International, iliishtumu serikali ya Syria kwamba imeendelea kutenda " uhalifu wa kivita " dhidi ya watu wa mkoa huo, ikisema kuhusu " mashambulizi ya moja kwa moja, yanayoendeshwa kiholela na katika mazingira yasioeleweka ".
Mashambulizi ya Jumapili yanakwenda sanjari na ziara ya mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu, Stephen O'Brien, ambaye anafanya ziara yake ya kwanza nchini humo.
Alipowasili Jumamosi, O'Brien alisema kuwa ziara yake inalenga " kutathmini mahitaji ya watu wa Syria ili waweze kupatishiwa misaada ya kibinadamu ", kulingana na tafsiri ya Kiarabu ya shirika la habari la serikali ya Syria, Sana.
O'Brien alisisitiza Jumamosi kwenye Twitter dhamira ya Umoja wa Mataifa kuendelea "kuunga mkono juhudi za kibinadamu nchini Syria ", nchi ambayo ina wakimbizi wa ndani milioni 7.6 na watu 422,000 walioyahama makaazi yao kufuatia mapigano kati ya pande zinazopigana kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya watu milioni nne wameikimbia nchi hiyo tangu mwaka 2011.