SYRIA-MAPIGANO-MAUAJI-USALAMA

Syria: watu 26 wauawa katika mashambulizi mawili

Magari yalioteketezwa kwa moto baada shambulio la kujitoa mhanga katika mji wa Latakia, Agosti 13, 2015, Syria
Magari yalioteketezwa kwa moto baada shambulio la kujitoa mhanga katika mji wa Latakia, Agosti 13, 2015, Syria AFP/SANA/AFP/Archives

Watu ishirini na sita waliuawa Ijumaa Septemba 4 katika mashambulizi mawili ya mabomu yaliotegwa katika magari mawili madogo Kusini mwa Syria.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi mmoja kutoka jamii ya Wadruze anayejulikana kuwa haiungi mkono serikali ya Bashar al-Assad na Waislam wenye msimamo mkali ni miongoni mwa watu waliuawa, Shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH), limebaini.

" Idadi ya watu waliouawakatika mashambulizi ya mabomu yaliotegwa katika magari madogi nje ya jiji la Suweida Ijumaa wiki hii imefikia 26, ikiwa ni pamoja na Sheikh muhimu kutoka jamii ya Wadruze. Watu wengine 50 wamejeruhiwa ", amesema Rami Abdel Rahman, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali, ambaye awali aliarifu kuwa watu wanane ndio waliuawa.

"Sheikh al-Wahid Balous aliuawa katika shambulio la bomu lililotegwa katika gari ndogo wakati alikua akiendesha gari nje kidogo ya mji wa Suweida ", Rami Abdel Rahman alisema mapema Ijumaa mchana.

Gari la pili iliotegwa bomu ililipuka karibu na hospitali ambapo watu waliojeruhiwa walisafirishwa, katika wilaya ya Jabal al-Dahr. Suweida ni ngome kuu ya watu wachache kutoka jamii ya Wadruze, ambayo inawakilisha karibu 3% ya raia wa Syria.

" Sheikh al-Balous alikuwa kiongozi wa kundi la 'Masheikh wa heshima', ambalo lilijipa jukumu la kulinda maeneo yanayokaliwa na watu wachache kutoka jamii ya Wadruze nchini Syria ", Malek Abu Kheir, mwandishi wa habari wa Suweida anayemtambua Balous, ameliambia shirika la habri la Ufaransa la AFP.

Kundi hili liliendesha vita dhidi ya kundi la Al-Nusra Front, tawi la Al Qaeda nchini Syria, ambapo wanachama wake walijaribu kujipenyeza ili kuingia katika jimbo la Suweida pamoja na kundi jingine la kijihadi la Islamic State (EI).