Zaidi ya watu 31 wauawa katika shambulio dhidi ya ngome ya waasi karibu na Damascus
Watu wasiopungua 31 wameuawa Jumapili hii na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio lililoendeshwa dhidi ya ngome ya waasi karibu na mji wa Damascus, shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH) limeleza.
Imechapishwa: Imehaririwa:
"Zaidi ya watu 31 waliuawa, wakiwemo watoto wawili, na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi ya anga yalioendeshwa katika mji wa Duma katika eneo la mashariki pamoja na makombora yaliyorushwa na vikosi vya serikali katika mji wa Duma na (kijiji cha) Saqba", Rami Abdel Rahman, ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP.
Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo, idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa sababu watu wengi waliojeruhiwa wako katika hali mbaya. "Moja ya mashambulizi hayo ya anga yameendesha katika eneo lililo karibu na shule katika mji wa Duma, na kuua mkurugenzi wa shule hilo", Rami Abdel Rahman ameongeza.
Katika wingu la vumbi, wanaume wamekua wakiwaondoa watoto kutoka katika mabaki ya majengo yaliobomolewa, kwa mujibu wa mpiga picha wa AFP, aliyetembelea eneo hilo. Picha zilizorushwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na kundi la wanaharakati wa mji wa Duma pia zinaonyesha watoto wengi wakiwa wamejeruhiwa vibaya wakiokolewa.
Mashambulizi pia ya anga yameendeshwa katika eneo la Hammouriyah Jumapili hii katika eneo la mashariki bila hata hivyo kusababisha vifo, shirika la Haki za binadamu (OSDH) limeeleza.
Duma, ngome ya waasi inayopatikana katika eneo la mashariki, mashariki mwa mji wa Damascus, imekua ikilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya ndege za kijeshi za Syria au za Urusi. Waasi pia huwa wakirusha mabomu kutoka mji huo hadi mji mkuu wa Syria, ambao ni ngome ya serikali.
Shirika la habari la Syria SANA limearifu kwamba "makundi ya kigaidi" yalirusha makombora katika maeneo ya mji mkuu Damascus yanayokaliwa na watu, na "kuua mtoto mmoja na kuwajeruhi watu watatu."
Mazungumzo yalioanzishwa mwezi Novemba kati ya makundi ya waasi na serikali kuhusu uwezekano wa kusitisha mapigano katika eneo la mashariki, lakini yalishindwa.