AFGHANISTAN-NATO-MAREKANI-TALIBAN-USALAMA

Afghanistan: askari 6 wa NATO wauawa katika shambulizi la Taliban

Wapiganaji wa kundi la Taliban wameendelea Jumatatu hii na harakati zao walioanzisha katika majira ya joto nchini kote Afghanistan ikiwa ni pamoja na mauaji ya kujitoa mhanga yaliowaua askari sita wa NATO karibu na mji wa Kabul na vita vikali kwa udhibiti wa wilaya muhimu katika ngome yao ya kusini ya Helmand.

Askari wa NATO wakipiga doria katika mji wa Kabul, Oktoba 11, 2015.
Askari wa NATO wakipiga doria katika mji wa Kabul, Oktoba 11, 2015. AFP/AFP
Matangazo ya kibiashara

Ikiwa imefikia karibu mwaka mmoja kwa kutamatika kwa jukumu la Umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi NATO kwa kuendesha vita nchini Afghanistan, wapiganaji wa kundi la Taliban wamezindisha mashambulizi yao walioanzisha baada ya utawala wao kuanguka mwaka 2001 kwa kuzidisha mashambulizi dhidi ya maeneo muhimu, ikiwa ni pamoja majeshi ya NATO na vikosi vya usalama vya Afghanistan.

Mauaji ya kujitoa mhanga kwenye pikipiki ambayo yamegharimu maisha ya askari sita wa kigeni kaskazini mwa Kabul Jumatatu hii, karibu na kambi ya Bagram, kambi kubwa ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan, ni moja ya ushahidi wa kuongezeka kwa mashambulizi hayo.

Askari hao waliouawa, ambao NATO haikutaja mataifa wanakotoka, walikuwa wakipiga doria na askari wa Afghanistan wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga kwenye pikipiki alipojilipua, amearifu Asem Muhammad, gavana wa jimbo la Parwan ambako kunapatikana kambi hiyo.

"Askari watatu wengine wa NATO wamejeruhiwa", muungano umesema katika taarifa yake.

kundi la Taliban lilikiri mara moja kuendesha shambulizi hilo na kudai kuwa "wanajeshi 19 wa Marekani wameuawa". Wapiganaji wa kundi la Taliban wamekua na tabia ya kuzidisha idadi au ukubwa wa mashambulizi yao dhidi ya vikosi vya kijeshi.