LEBANONO-ISRAEL-UHASAMA

Mauaji ya Samir Kantar yazua hali ya taharuki kati ya Israel na Lebanon

Hali ya taharuki imepanda kati ya Israel na Lebanon Jumapili jioni baada ya kifo cha kiongozi muhimu anayeheshimika katika kundi la Hezbollah, Samir Kantar, ambaye aliuawa Jumamosi katika mashambulizi ya anga ya Israel karibu na mji wa Damascus.

Jengo lililolengwa na mashambulizi ya anga ya Israel ambapo Samir Kantar, kiongozi muhimu wa kundi la Hezbollah, aliuawa karibu na mji wa Damascus.
Jengo lililolengwa na mashambulizi ya anga ya Israel ambapo Samir Kantar, kiongozi muhimu wa kundi la Hezbollah, aliuawa karibu na mji wa Damascus. AFP PHOTO / LOUAI BESHARA
Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Israel lilijibu mashambulizi ya kundi hili baada ya kuanguka kwa makombora kadhaa kaskazini mwa Israel, kwa kurusha makombora kusini mwa Lebanon, na ndege za Israel zilipaa katika anga ya mji wa Beirut na sehemu ya kusini mwa Lebanon.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI, mjini Beirut, Paul Khalifeh makombora manane ya Israel yalirushwa kusini mwa mji wa bandari wa Tyr kusini mwa Lebanon, bila kusababisha majeruhi. Makombora hayo yalilenga eneo kulikokua kukirushwa makombora, upande wa Lebanon, Jumapili hii alaasiri. Makombora ambayo yalirushwa kutoka upande wa pili, kaskazini mwa Israel. Wakati huo huo, ndege za kivita za Israel zilipaa katika anga ya sehemu ya kusini mwa Lebanon na katika kitongoji cha kusini mwa mji wa Beirut, ambacho ni ngome ya kundi la Hezbollah.

Matukio haya yalitokea baada siku moja ya kifo cha Samir Kantar, kiongozi muhimu anayeheshimika katika kundi la Hezbollah, ambaye aliuawa Jumamosi usiku na mashambulizi ya anga ya Israel katika mji wa Jaramana, kusini mwa mji wa Damascus. Samir Kantar alifungwa miaka thelathini katika magereza ya Israel kabla ya kuachiliwa huru mwezi Julai 2008 katika utaratibu wa kubadilishana wafungwa.

Tangazo la Hassan Nasrallah

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari mjini Beirut, habusu huyo wa zamani alikua anahusika na mafunzo kwa makundi yanayopinga Israel katika milima ya Golani nchini Syria, eneo lililodhibitiwa na Israel mwaka 1967. Samir Kantar ni kutoka jamii ya Wadruze, kama wakazi wengi wa Ukanda huo. Hali hiyo ilimpelekea kuimarisha mawasiliano yake na kusajili vijana wengi kutoka jamii hiyo. Maofisa kadhaa wa kundi aliloanzisha wameuawa pamoja naye.

Samir Kantar ni mmoja wa viongozi wa kuu wa kundi la Hezbollahambao wameuawa nchini Syria. Kiongozi wa kundi, Hassan Nasrallah, anatazamiwa kutoa hotuba leo Jumatatu jioni ili kuelezea kifo chake.