SYRIA-UPINZANI-SIASA

Syria: wapinzani wawili wakamatwa

Serikali ya Syria imewatia mbaroni Jumatano hii wanasiasa wawili wa upinzani, wanaoishi nchini humo, ambao hivi karibuni walihudhuria mkutano mjini Riyadh na wapinzani wa kisiasa na makundi ya waasi.

Picha ilitolewa na shirika la habari la Saudia Arabia, Desemba 10, 2015 ikimuonyesha Waziri wa mambo ya ndani Mohammed Bin Nayef (katikati kulia) na Waziri wa Ulinzi Mohammed bin Salman (kushoto) wakiwakaribisha wajumbe wa upinzani wa Syria.
Picha ilitolewa na shirika la habari la Saudia Arabia, Desemba 10, 2015 ikimuonyesha Waziri wa mambo ya ndani Mohammed Bin Nayef (katikati kulia) na Waziri wa Ulinzi Mohammed bin Salman (kushoto) wakiwakaribisha wajumbe wa upinzani wa Syria. AFP/AFP/
Matangazo ya kibiashara

Mamia ya wawakilishi wa vyama vikuu vya kisiasa na upinzani kutoka makundi yenye silaha walitangaza Desemba 10 makubaliano yao kwa ajili ya mazungumzo na serikali, hata hivyo wakidai kuondoka madarakani kwa Rais Bashar al-Assad pamoja na kuanza kwa kipindi cha mpito.

Ahmed al-Asrawi na Mounir al-Bitar, wanasiasa wawiwili vigogo nchini humo, "wamekamatwa na serikali ya Syria katika mpaka na Lebanon", Katibu mkuu wa chama cha wanasiasa hao ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP.

Wote wawili walishiriki katika mkutano wa mjini Riyadh na ni miongoni mwa wajumbe wa "Kamati kuu" ya upinzani, taasisi iliyoundwa kwa minajili ya mkutano huo kwa kujiandaa kwa ajili ya uwezekano wa mazungumzo na serikali.

Jumatano hii, walikuwa njiani kwenda Saudi Arabia, ambapo wangelihudhuria mkutano mpya wa Kamati kuu, kwa mujibu wa Bw. Aziz ambaye amebaini kwamba wapinzani wote hao wawili wamehamishiwa katika "eneo kusikojulikana".

Umoja wa Mataifa unatarajia kuwa mazungumzo yazinduliwa mnamo Januari 25 mjini Geneva. Utawala wa Damascus hivi karibuni ulitangaza utayari wake wa kushiriki katika mazungumzo hayo, ukibainisha hata hivyo kuwa unasubiri kujua ni makundi gani ya upinzani ambayo yatashiriki katika mazungumzo hayo.