YEMENI-MAPIGANO-USALAMA-SIASA

Yemen: watu sita wauawa katika mapigano kati ya Al-Qaeda na jeshi

Wanamgambo wenye silaha kutoka makundi yanayoshirikiana na vikosi vya serikali tiifu kwa rais Abdrabbo Mansour Hadi wakirusha risasi katika mkoa wa Sirwah nchini Yemen, Desemba 18, 2015.
Wanamgambo wenye silaha kutoka makundi yanayoshirikiana na vikosi vya serikali tiifu kwa rais Abdrabbo Mansour Hadi wakirusha risasi katika mkoa wa Sirwah nchini Yemen, Desemba 18, 2015. AFP/AFP/

Watu sita wameuawa Ijumaa hii katika urushianaji risasi kati ya vikosi vya serikali vya Yemen na wapiganaji wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al Qaeda ambao wamekuwa wakielekea katika mji wa pili wa Aden, kwa mujibu wa maafisa wa usalama.

Matangazo ya kibiashara

Makabiliano ya kijeshi yamezuka wakati ambapo wanamgambo wanaoiunga mkono serikali waliokua wakidhibiti kituo cha ukaguzi katika mkoa wa Abyan (kusini) walipowakamata watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi ambao walikua wakitembea kwa gari la kivita, vyanzo vya usalama vimebaini.

Watu watatu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Al Qaeda na wanamgambo kadhaa wanaoiunga mono serikali wameuawa.

Mkuu wa mahakama iliyoanzishwa na Al Qaeda katika mji wa Mukalla, kusini mwa Yemen, mji unaodhibitiwa na kundi la kijihadi tangu mwezi Aprili, ni miongoni mwa watu waliouawa, maafisa wa usalama wamesema.

Yemen imeendelea kukumbwa na mapigano tangu mwezi Aprili kati ya vikosi vya serikali vinavyosaidiwa na muungano wa Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa Kishia wa Huthi wanaoungwa mkono na Iran ambao wanaendelea kuushikilia mji mkuu wa Yemen, Sanaa, tangu mwezi Septemba 2014 kabla ya kuyateka maeneo mengine kusini mwa nchi hiyo.

Hali imeendelea kuwa mbaya kufuatia kuongezeka kwa makundi ya Waislamu wenye msimamo mkali katika miezi ya hivi karibuni, wakichukulia hali ya machafuko inayoendelea kushuhudiwa nchini humo kwa kuimarisha ngome zao, hasa kusini mwa Yemen.

Mji wa Aden, ambao ulitangazwa hivi karibuni kama mji mkuu wa muda, unaendelea kukabiliwa na mapigano kati ya makundi hasimu ya wanajihadi, Al Qaeda, iliokita mizizi kwa miaka kadhaa, na kundi la Islamic State (IS).

Waislamu wenye msimamo mkali wamedhibiti majengo kadhaa ya serikali na wamekua wakiendesha mashambulizi makali dhidi ya maafisa wa serikali.

Tangu mwezi Machi, vita nchini Yemen vimesababisha vifo vya watu 6,000 na wengine 28,000 kujeruhiwa, huku watu milioni 2.5 wakiyahama makazi yao.