ISRAEL-MASHAMBULIZI

Askari 2 wajeruhiwa kwa risasi katika Ukingo wa Magharibi

Askari wawili wa Israel wamejeruhiwa kwa risasi katika mashambulizi mawili Jumapili hii kusini mwa Ukingo wa Magharibi, jeshi limesema.

Askari wa Israel kwenye eneo la mashambulizi ya silaha dhidi ya askari mwanamke wa Israel katika eneo laHebroni katika Ukingo wa Magharibi, 3 Januari 2016.
Askari wa Israel kwenye eneo la mashambulizi ya silaha dhidi ya askari mwanamke wa Israel katika eneo laHebroni katika Ukingo wa Magharibi, 3 Januari 2016. AFP/AFP
Matangazo ya kibiashara

Askari mmoja amejeruhiwa vibaya kwa risasi lililorushwa na mtu ambaye hakujulikana karibu na pango la kale katikati mwa mji wa Hebroni, jeshi limebaini katika taarifa yake. Askari huyo mwanamke amepelekwa hospitali ya Shaare Tzedek katika mji wa Jerusalem, kwa mujibu wa msemaji wa hospitali.

Muda wa saa tatu baadaye, askari mwengine amejeruhiwa kidogo kwa risasi wakati askari waliokua wakipiga doria waliposhabuliwa kusini mwa mji wa Hebroni lakini mshambuliaji aliweza kukimbia, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi.

Jeshi halijasema kama washambuliaji walikuwa Wapalestina, wakati ambapo eneo la Hebroni limekua likikabiliwa na mashambulizi kadhaa ya Wapalestina dhidi ya Waisrael katika wiki za hivi karibuni.

Takriban walowezi 500 wa Kiyahudi wanaishi katika eneo la Hebroni lilio chini ya ulinzi mkali wa jeshi la Israel miongoni mwa Wapalestina 200,000 waishio eneo hilo.

Jumamosi Januari 2, maelfu ya watu walizika miili 14 ya Wapalestina ambapo Israeli ilikabidhi miili kwa ndugu zao katika eneo la Hebroni. Wapalestina hawa walipigwa risasi wakati walikua wakiwashambulia au wakijaribu kuwashambulia Waisrael.

Mashambulizi haya ya Jumapili yanatokea katika mazingira ya wimbi la machafuko yaliosababisha vifo vya Wapalestina 138 na Waisrael 20 tangu Oktoba 1, 2015. Wengi wa Wapalestina waliouawa wanachukuliwa na Israel kama washambuliaji.