SAUDIA ARABIA-IRAN-USHIRIKIANO

Riyadh na washirika wake wavunja uhusiano na Iran

Saudi arabia ikiwaonyesha wafanyakazi wa ubalozi wake mjini Tehran wakirejea nchini mwao, Januari 4, 2016.
Saudi arabia ikiwaonyesha wafanyakazi wa ubalozi wake mjini Tehran wakirejea nchini mwao, Januari 4, 2016. AL-IKHBARIYA TV/AFP

Mvutano kati ya Iran na majirani zake Waarabu wa Kisuni umeibuka Jumatatu hii, baada ya Saudi Arabia na washirika wake kuvunja au kupunguza uhusiano wa kidiplomasia na Tehran baada ya mgogoro uliosababishwa na mauaji ya mhubiri wa Kishia.

Matangazo ya kibiashara

Urusi, imesema kuwa inatiwa "wasiwasi" na hali hiyo, na kubaini kwamba iko "tayari kusaidia" mazungumzo kati ya Riyadh na Tehran, nguzo mbili za ushawishi katika Ukanda wa Mashariki ya Kati unaokabiliwa na machafuko.

Marekani, ambayo ni mshirika wa Saudi Arabia lakini hivi karibuni ilifufua uhusiano na Iran kufuatia makubaliano ya nyuklia mwezi Julai, imezitaka nchi hizo mbili kuchukua "hatua chanya kwa kutuliza mvutano huo."

Ufaransa na Ujerumani pia wametoa wito wa kukomesha mvutano huo baada ya Bahrain na Sudan, kama Riyadh, kutangaza kuvunja mahusiano ya kidiplomasia na Iran. Umoja wa Falme za Kiarabu uliomuitisha balozi wake mjini Tehran umepunguza mahusiano yake ya kidiplomasia na Iran.

Mgogoro mpya ulizuka Jumamosi kufuatia mauaji ya mhubiri wa Kishia Nimr al-Nimr, pamoja na watu wengine 46 waliohukumia kwa kosa la "ugaidi". Mauaji hayo yalitekelezwa na utawala wa Kisuni wa Saudi Arabia.

Mauaji hayo yamesababisha vita vya maneno kati ya Tehran na Riyadh pamoja na maandamano yaliojaa hasira miongoni mwa jamii ya Mashia katika nchi kadhaa ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na Iran ambapo balozi za Saudi Arabia zimeshambuliwa, Iraq, Lebanon, Bahrain, Pakistan pamoja na Kashmir nchini India.

Jumapili jioni, Saudi Arabia ilitangaza "kuvunja mahusiano ya kidiplomasia na Iran na kuamuru ujumbe wa balozi za Iran kuondoka nchini humo ndani ya masaa 48."