ISRAEL-PALESTINA-MASHAMBULIZI

Visa vya mashambulizi ya visu vyaendelea katika Ukingo wa Magharibi

Askari wa Israel akitoa ulinzi katika eneo la Gush Etzion, katika Ukingo wa Magharibi, Januari 5, 2016.
Askari wa Israel akitoa ulinzi katika eneo la Gush Etzion, katika Ukingo wa Magharibi, Januari 5, 2016. AFP/AFP

Raia mmoja wa Palestina amemjeruhi kwa kisu Jumanne hii askari wa Israel karibu na eneo la Gush Etzion, katika Ukingo wa Magharibi, kabla ya kupigwa risasi na vikosi vya Israel viliokua eneo hilo, jeshi la Israel limesema.

Matangazo ya kibiashara

Askari, aliyeonyeshwa na jeshi kama askari wa ziada, amepelekwa hospitali akiwa na majeraha usoni na mkononi, maafisa wa Idara za huduma za dharura wamesema.

Mshambuliaji ametambuliwa na Wizara ya Afya ya Palestina kama Kawazbeh Ahmed, mwenye umri wa miaka 18, kutoka kijiji cha Sair, karibu na mji wa Hebroni kusini mwa Ukingo wa Magharibi.

Shambulio hili ni la mwisho katika mfululizo wa mashambulizi kadhaa, hasa kwa visu, yaliotekelezwa kwa muda wa wiki kadhaa na Wapalestina dhidi ya Waisrael katika Ukingo wa Magharibi, Jerusalem na Israel.

Eneo la Gush Etzion limeendelea kushuhudia mashambulizi dhidi ya Waisral.

Mashambulizi na makabiliano kati ya Wapalestina na vikosi vya usalama vya Israel yamesababisha vifo vya Waisrael 22 na Wapalestina 139 tangu Oktoba 1, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Idadi kubwa ya Wapalestina waliouawa walitekeleza mashambulizi au walionyeshwa na Israeli kama washambuliaji kwa kutumia visu.

Raia mmoja kutoka Marekani na raia mwengine mmoja kutoka Eritrea pia waliuawa katika ghasia hizo.