SAUDIA ARABIA-IRAN-USHIRIKIANO

Nchi za Kiarabu zaiunga mkono Saudi Arabia

Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry kulia) na mwenzake wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir (kushoto), Januari 10, 2016, Cairo.
Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry kulia) na mwenzake wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir (kushoto), Januari 10, 2016, Cairo. AFP/AFP

Nchi za Umoja wa Kiarabu zimeonyesha Jumapili hii "mshikamano" kwa Saudi Arabia kukabiliana na "vitendo vya uadui" vya Iran, wakati ambapo mgogoro mkubwa wa kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili unaendelea kushuhudiwa.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, Riyadh imesema inaunga "mkono kikamilifu" mazungumzo kuhusu mgogoro wa Syria, ambao unatazamiwa kuanzishwa mwishoni mwa mwezi Januari, saa chache baada ya Waziri wa mambo ya nje wa Iran kuishtumu Riyadh kutaka "kuathiri" mazungumzo hayo.

Hayo yanajiri wakati Riyadh na Tehran, mataifa mawili yanayohusika katika vita nchini Syria lakini pia katika migogoro mingine ya kikanda, yanatupiana vijembe tangu mauaji ya mhubiri kutoka jamii ya Mashia Nimr al-Nimr Januari 2 nchini Saudi Arabia. Nimr al-Nimr alikua kiongozi mkuu wa upinzani wa kisiasa ambaye alihukumiwa kwa kosa la "ugaidi."

Mauaji yake yalisababisha maandamano na mashambulizi dhidi ya balozi za Saudi nchini Iran, hali ambayo ilipelekea Riyadh kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Tehran.

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka Umoja wa nchi za Kiarabu wamekusanyika Jumapili hii mjini Cairo, na kuonyesha msikamano wao kwa Saudi Arabiadhidi ya "vitendo vya uhasama na chuki vya Iran."

Umoja wa nchi za Kiarabu umelaani tangazo la Iran dhidi ya Saudi Arabia na kutaja kuwa, kuhusu mauaji ya mhubiri wa kishia, Iran imekiuka sheria kwa "kuingilia" masuala ya ndani ya utawala wa kifalme wa " Saudi Arabia".

Jumamosi hii, Baraza la Ushirikiano la nchi za Ghuba (GCC) liliiunga mkono Saudi Arabia, na kutishia "kuchukua hatua zaidi dhidi ya Iran kama nchi hiyo itaendelea vitimbi vyake dhidi ya Saudi Arabia."