IRAQ-SHAMBULIO-MAUAJI

Iraq: watu 8 wauawa katika jumba la biashara Baghdad

Watu wenye silaha wamelipua Jumatatu hii bomu lililokua limetegwa katika gari na kurusha risasi katika eneo linalotembelewa na watu wengi mjini Baghdad kabla ya kuwashikilia watu mateka katika jumba la biashara, na kuua watu wasiopungua wanane, polisi imesema.

Askari polisi wa Iraq mbele ya bendera ya Iraq, katika mji wa Najaf Januari 9, 2016.
Askari polisi wa Iraq mbele ya bendera ya Iraq, katika mji wa Najaf Januari 9, 2016. AFP/AFP/
Matangazo ya kibiashara

Washambuliaji walikuwa bado katika jumba hilo la biashara katika eneo la mji wa Baghdad la Al-Jadida, mashariki mwa mji mkuu, kwa mujibu wa afisa wa polisi, ambaye amesema washambuliaji hao wanaweza kuwa wamevaa mikanda iliyojaa vilipuzi.

"Wapo katika jumba la biashara la Zahrat. Wakati vikosi vya usalama viliwakaribia, waliwaua mateka watatu", afisa huyo wa polisi amesema. "Kwa sasa tunachukua njia ya tahadhari. Tunataka kukomesha shambulio hili kwa kuzuia maafa makubwa ambayo yanaweza kutokea."

Chanzo cha kitabibu kimethibitisha idadi ya watu wanane waliouawa, kikiongeza kuwa watu 14 pia wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Jumba hilo la biashara ni jengo la ghorofa nne au tano lililojengwa katika eneo linalotembelewa na watu wengi, hasa Mashia, mashariki mwa mji mkuu wa Iraq.

Kwa mujibu wa chanzo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, idadi isiyojulikana ya watu wenye silaha wamerusha risasi mitaani baada ya mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa katika gari, na wamekabiliana kwa muda mfupi na vikosi vya usalama kabla ya kuingia katika jumba hilo la Biashara.

"Kwa sasa washambuliaji hao wanadhibiti jumba lote la biashara na baadhi ya watu wenye silaha wako kwenye paa", afisa wa polisi ameongeza.

Polisi inasema vikosi vya kupambana na ugaidi na maafisa wa Idara ya Ujasusi wametumwa eneo hilo na wako pembezoni mwa jumba la biashara la Zahrat.

Hakuna kundi ambalo, kwa sasa, limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini chanzo cha polisi kinabaini kwamba washambuliaji "wamevaa kama wapiganaji wa kundi la Isalmic State".