SYRIA-IS-MAUAJI

Syria: kundi la IS latekeleza mauaji karibu na Deir Ezzor

Maelfu ya raia ambao bado wanaishi katika sehemu ya jimbo la Deir Ezzor na vijiji jirani vilio chini ya udhibiti wa vikosi vya serikali.
Maelfu ya raia ambao bado wanaishi katika sehemu ya jimbo la Deir Ezzor na vijiji jirani vilio chini ya udhibiti wa vikosi vya serikali. REUTERS/Khalil Ashawi

Jumamosi januari 16, 2016, kundi la Islamic State liliwaua, watu wasiopungua 135, ikiwa ni pamoja na raia wa kawaida 85 na askari 50 wa serikali karibu na mji wa Deir Ezzor, mashariki mwa Syria, kwa mujibu wa shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH).

Matangazo ya kibiashara

Katika jimbo la Aleppo, jeshi la Syria linaelekea kwenye ngome kuu ya kundi la IS.

Kundi la Islamic State limetekeleza mauaji makubwa katika kijiji cha Baghiliyya nje kidogo ya mji wa Deir Ezzor, mji mkuu wa jimbo la Deir Ezzor, mashariki mwa Syria. Shirika la habari la serikali limearifu kuwa watu 280 waliuawa. Idadi ambayo imethibitishwa na vyanzo huru mjini Damascus, amearifu mwandishi wetu mjini Beirut, Paul Khalifeh.

Wanawake wengi na watoto kutoka familia nzima za askari wa serikali ni miongoni mwa watu waliouawa kwa risasi au kuchinjwa. Miili yao imetupwa ndani chimo. Wakazi 400 wa kijiji hicho kinachokaliwa na watu wengi kutoka jamii ya Wasuni, ambao wanaunga mkono serikali, wanadaiwa kutekwa nyara na kundi la Islamic State.

Washambuliaji wa kujitoa mhanga

Mashambulizi dhidi ya kijiji hiki yalianza na wimbi la kwanza la washambuliaji thelathini wa kujitoa mhanga, ambao walishambulia ngome za jeshi la Syria. Kisha mamia ya wapiganaji waliingilia kati, na kuwatimua askari wa serikali, na hivyo kuiteka sehemu kubwa ya kijiji hicho.

Mashambulizi hayo yalipelekea kundi la Islamic State kusonga mbele kaskazini mwa mji mkuu uliogawanyika wa jimbo hilo lenye utajiri wa mafuta. Karibu 60% ya mji huo umeanguka mikononi mwa kundi la IS. Na licha ya mashambulizi ya mara kwa mara ya wanajihadi, serikali bado inadhibiti sehemu ya jimbo la Deir Ezzor na uwanja wa ndege wa kijeshi ulio jirani. Maelfu ya raia bado wanaishi katika eneo la mji na vijiji jirani.

Jeshi la serikali lasonga mbele katika jimbo la Aleppo

Katika jimbo la Aleppo, jeshi la Syria linasonga mbele dhidi ya kundi la IS. Kwa sasa liko kilomita sita tu kutoka mji wa Al-Bab, ngome kuu ya kundi la kigaidi katika jimbo hilo.

Likisaidiwa na mamia ya mashambulizi ya anga ya Urusi, jeshi la Syria limeyarejesha nyuma mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la Islamic State ambalo limepoteza wapiganaji zaidi ya ishirini.