PAKISTAN-SHAMBULIO-USALAMA

Pakistan: Chuo kikuu chashambuliwa na watu wenye silaha

Vikosi vya usalam vikiendesha operesheni ya kuwatimua watu wenye silaha waliovamia Chuo kiku Pakisan. Operesheni ikirushwa moja kwa moja kwenye runinga ya serikali.
Vikosi vya usalam vikiendesha operesheni ya kuwatimua watu wenye silaha waliovamia Chuo kiku Pakisan. Operesheni ikirushwa moja kwa moja kwenye runinga ya serikali. REUTERS/ARY News

Watu wasiopungua 21 wameuawa katika shambulio la watu wenye silaha wasiojulikana Jumatano hii dhidi ya Chuo kikuu kaskazini magharibi mwa Pakistan, na kuwajeruhi watu wengi, Naibu mkuu wa Chuo kikuu hicho ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP, akiongeza kwamba shambulio bado linaendelea.

Matangazo ya kibiashara

Watu wenye silaha "wameweka ngome yao katika Chuo kikuu na milio ya risasi inaendelea kusikika katika Chuo kikuu hicho", amesema Fazal Raheem Marwat, Naibu mkuu wa Chuo kikuu cha Bacha Khan katika mji wa Charsadda, mji ulio kwenye kilomita hamsini kutoka Peshawar.

Kundi la Taliban nchini Pakistan limekiri kuhusika na shambulio hilo. "Washambuliaji wetu wanne wa kujitoa mhanga wameendesha leo mashambulizi dhidi ya Chuo Kikuu cha Bacha Khan", mkuu wa wapiganaji, Umar Mansoor, amsema alipohojiwa kwa simu na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Naibu mkuu wa Chuo kikuu hicho amesema amepata taarifa ya shambulio hilo kutoka kwa polisi, wakati ambapo alikua njiani akielekea kazini. Mpaka sasa watu 21 ndio wanasadikiwa kuwa wameuawa, huku wengine wengi ikiwa ni pamoja na walinzi wa Chuo kikuu hicho wamejeruhiwa.

"Wafanyakazi, wanawake na wanaume, pamoja na wanafunzi wamejificha katika mabweni ya Chuo kikuu", ameongeza Fazal Raheem Marwat. Chuo kikuu hiki kilikua bado hakijakumbwa na mashambulizi ya aina yoyote mpaka sasa, "lakini tulikuwa tuliimarisha ulinzi katika Chuo kikuu hicho."

Mashambulizi mabaya yaliotokea nchini humo mwaka mmoja uliopita katika shule ya msingi ya Peshawar, iliovamia na wapiganaji wa Taliban ambao waliua kinyama zaidi ya watu 150, wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule hiyo, wakati wa mashambulizi yaliyodumu saa kadhaa.

Kwa sababu hiyo, idadi ya mashambulizi imeshuka kwa kiasi kikubwa mwaka 2015. Hata hivyo Jumanne hii, shambulio la kujitoa mhanga katika mji wa Peshawar liliwaua watu 10.