SYRIA-MAZUNGUMZO

Syria: maandalizi magumu kwa mkutano wa Geneva

Hakuna tangazo rasmi ambalo limetolewa, lakini ni wazi kuwa mkutano kuhusu Syria uliopangwa kufanyika Jumatatu hii, Januari 25 mjini Geneva utacheleweshwa na haijulikani ni lini utaanza.

Mji wa waasi wa Madaya, kusini magharibi mwa Syria, umezingirwa kwa miezi sita na jeshi la Bashar Al Assad.
Mji wa waasi wa Madaya, kusini magharibi mwa Syria, umezingirwa kwa miezi sita na jeshi la Bashar Al Assad. REUTERS/Omar Sanadiki
Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo ya amani yaliyotayarishwa na Umoja wa Mataifa yatawakutanisha wawakilishi wa upinzani na serikali ya Bashar al-Assad.

Upande wa upinzani wa Syria wanasema, ni vigumu kuzungumza wakati ambapo mashambulizi ya Urusi yanaendelea, na maeneo kadhaa yamezingirwa na jeshi la serikali ya Damascus. Pia ni vigumu kukaa kwenye meza ya mazungumzo kama ajenda haitoweka wazi kipindi cha mpito nchini Syria, na kuondoka madarakani kwa Bashar al-Assad.

Bila dhamana ya kisiasa na kibinadamu, upinzani nchini Syria unaweza ukapoteza uaminifu ukisafiri kwenda Geneva. Upande wa serikali ya Syria na washirika wake, wanabaini kwamba wana wasiwasi na watu watakaounda ujumbe wa upinzani.

Kwa uhakika, ujumbe wa upinzani nchini Syria unaundwa na makundi ya waasi wenye silaha, na serikali ya Damascus inakataa kujadili na baadhi ya makundi hayo, kwa kuanzia kwa Jeshi la Uislamu, kundi la waasi wa Salafi, ambapo mmoja wa viongozi wake, Mohammed Alloush, aliteuliwa kushiriki katika mazungumzo hayo na muungano wa vyama vya upinzani.

Wakati huo huo, Urusi inataka makundi mengine ya upinzani, ikiwa ni pamoja na Wakurdi wa Syria waweze kuwakilishwa katika mkutano wa Geneva, ombi ambalo linapingwa na muungano wa sasa wa wapinzani wa Bashar Assad.