SYRIA-MAZUNGUMZO

Mazungumzo kuhusu Syria yaanza Ijumaa Geneva

Mazungumzo yenye lengo la kukomesha vita nchini Syria yataanza mjini Geneva Ijumaa hii Januari 29, msemaji wa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura ametangaza Alhamisi hii, ingawa makundi yote ya upinzani bado hayajatangaza kuwa yatashiriki katika mazungumzo hayo.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura, Januari 15 mjini Geneva.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura, Januari 15 mjini Geneva. REUTERS/Pierre Albouy
Matangazo ya kibiashara

"Ninathibitisha tu kwamba mazungumzo yataanza Ijumaa", amesema Khawla Mattar, msemaji wa Ofisi ya Staffan de Mistura kwa jibu aliloandika kupitia barua pepe.

Muda mfupi kabla, Ofisi ya Staffan de Mistura ilitoa ujumbe wa video kwa raia wa Syria, ambapo ilisema kuwa mazungumzo huenda yakafanyika "katika siku zijazo."

Mwanzoni mwa wiki hii Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura alitangaza kwamba alituma mialiko kwa "wajumbe mbalimbali kutoka Syria" watakaoshiriki mazungumzo hayo Ijumaa wiki hii, bila hata hivyo kubainisha watu watakao shiriki mazungumzo hayo. Hata hivyo mpaka sasa bado pande zote hawajaafikiana kufusu muundo wa ujumbe wa upinzani.

Kwa upande wake Uturuki ilisema wiki hii kwamba hatoshiriki katika mazungumzo ya amani ya Syria yatakayoanza mjini Geneva siku ya Ijumaa kama chama cha PYD cha Wakurdi kutoka Syria hakitoshiriki, ameonya Jumanne hii Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu.