SYRIA-MVUTANO-MASHAMBULIZI

Syria: mvutano waongezeka kati ya washirika na wapinzani wa Damascus

Mpiganaji wa jeshi la Syria akitoa ulinzi akiwa na silaha yake ya kaskazini mwa Aleppo, Januari 18, 2016.
Mpiganaji wa jeshi la Syria akitoa ulinzi akiwa na silaha yake ya kaskazini mwa Aleppo, Januari 18, 2016. REUTERS / Abdel Rahman Ismail

Pamoja na ahadi ya kusitiha mapigano, utatuzi wa mgogoro wa Syria umeonekana Jumapili hii kuingiliwa na hali ya sintofahamu, huku wahusika mbalimbali wa kimataifa, ikiwa ni pamoja Uturuki na Urusi, wanatuhumiana kila mmoja kuchochea machafuko.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Uturuki limeendesha mashambulizi ya mabomu Jumapili hii kwa siku ya pili mfululizo dhidi ya ngome za wapiganaji wa Kikurdi, kaskazini mwa Syria, karibu na mji wa Syria wa Azaz katika jimbo la Aleppo.

Serikali ya Syria imelaani "mashambulizi ya mara kwa mara ya Uturuki dhidi ya (...) taifa la Syria", ikitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, "kukomesha uhalifu wa serikali ya Uturuki".

Ikiendesha mashambulizi mapya, serikali ya Ankara imepuuzia wito wa "kukomesha mapigano" uliyotolewa na Marekani, mshirika wake wa karibu katika Umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi (NATO).

Uturuki imekua ikieleza mara kwa mara kuchanganyikiwa na msaada wa kijeshi unaotolewa na Washington kwa makundi ya Kikurdi, ikiwa ni pamoja na kundi linalokusanya vikosi vya ulinzi wa raia (YPG). Serikali ya Uturuki inahofia kwamba kundi hili, ambalo tayari limedhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Syria, linapania kudhibiti eneo nzima la mpakani.

Kusonga mbele kwa kundi la YPG magharibi mwa mto nchini Syria ni "mstari mwekundu", Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki Yalcin Akdogan, amesema. "Hili ni suala linaloathiri usalama wa taifa (...) Uturuki siyo taifa ambalo litaendelea kushuhudia bila kuchukua hatua", Akdogan ameonya.

- Ndege za Saudi Arabia Uturuki -

Licha ya kuipinga serikali ya Bashar al-Assad ambayo ina uhusiano mzuri na Urusi, Uturuki pia inapanga kuanzisha na Saudi Arabia operesheni ya kijeshi nchini Syria, operesheni yenye lengo la kupambana dhidi ya wanajihadi wa kundi la Islamic State(IS), kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu.

Vikosi "maalum" vya Saudi Arabia vinaweza kupelekwa kama sehemu ya muungano dhidi ya wanajihadi unaoongozwa na Marekani, Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir, ametangaza Jumapili hii bila kutoa maelezo zaidi.

Wakati huo huo Rais wa Marekani Barack Obama amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kujadili hali nchini Syria, Kremlin imetangaza Jumapili Februari 14. Mahojiano kati ya wawili hao yamekwenda "vizuri". Lakini hali ni tete nchini Syria.

Viongozi hao wawili wametoa "tathmini chanya" ya makubaliano ya usitishwaji wa uhasama nchini Syria uliyoamuliwa katika mkutano wa mjini Munich juma hili. Wote wawili "wamekubaliana kuendelea na ushirikiano kupitia njia za kidiplomasia na njia zingine ili kutekeleza makubaliano" ya mjini Munich, taarifa kutoka Kremlin imesema.